Gari la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadick likiwasili Dampo kuu la taka la Pugu Kinyamwezi,
lililopo maeneo ya Gongo la Mboto jijini Dar alipofanya ziara ya ghafla
kwenye dampo hilo.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Na. Damas Makangale, MOblog
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadick ametoa agizo mara moja kwa uongozi wa Dampo nje kidogo la jiji la
Dar, Pugu Kinyamwezi, kurekebisha miundombinu ya barabara pamoja na taa
ili kurahisisha umwagaji wa taka katika dampo hilo. MOblog inaripoti
Akizungumza na baadhi ya viongozi wa
wilaya na jiji hivi karibuni baada ya kufanya ziara ya ghafla katika
maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa amesema tatizo la
miundombinu ya barabara kuelekea katika Dampo la Pugu Kinyamwezi
linasababisha foleni kwa malori ya kusomba taka katika jiji la Dar.
“mara ya mwisho wakati nakuja hapa
kukagua hili dampo kulikuwa na taa na kazi ilikuwa inafanyika usiku na
mchana sasa kumetokea nini,” alihoji Mkuu huyo wa Mkoa
Sadick aliagiza kwa viongozi wa jiji
kushughulikia haraka tatizo la miundombinu ya barabara kuelekea Dampo
ili kuongeza tija katika kazi ya kumwaga na kusomba taka katika jiji la
Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Udhibiti taka
kutoka halmashauri ya jiji, Bi. Enezael Ayo (kushoto) akifafanua jinsi
magari ya taka yanavyomwaga taka katika dampo kuu taka la Pugu
Kinyamwezi jijini Dar wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Dar.
Alisisitiza kwamba utaratibu mbovu wa
umwagaji taka na miundombinu mibovu katika Dampo la Pugu Kinyamwezi
vinasababisha mrundikano wa taka katika manispaa zote za Temeke, Ilala
na Kinondoni.
Amesema kwamba ni muhimu kwa viongozi wa
jiji kupata nguvu kazi ya kutosha ili kuwe na watu watakaosimamia
umwagaji wa taka wakati wa usiku ili kudhibiti madereva wakorofi
wanaomwaga taka ovyo bila kuzingatia taratibu.
Sadick aliongeza kuwa watendaji wa jiji
ni lazima wawe na utaratibu wa kutoa mafuta kwa wakati kwenye magari ya
kusomba (Bull Dozer) na vitendea kazi vingine.
Mkuu wa mkoa wa Dar, Said Meck Sadick
akitoa agizo mara moja kwa uongozi wa Dampo nje kidogo la jiji la Dar,
Pugu Kinyamwezi, kurekebisha miundombinu ya barabara pamoja na taa ili
kurahisisha umwagaji wa taka katika dampo hilo. Mkuu wa Mkoa aliambatana
na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ndg. Raymond Mushi(mwenye suti nyeusi).
Wakati akitembelea maeneo kadhaa kati
kati ya jiji kuanzia soko la Kisutu na mitaa ya Libya, Mkuu wa Mkoa
aliagiza mamlaka zinazohusika kushughulikia haraka tatizo la maji
machafu kupunguza harufu na kuzuia magonjwa ya mlipuko.
“nawaagiza mkae pamoja na mje na mpango
mkakati utakaowezesha kumaliza tatizo la maji machafu yanayotoka katika
mitaro na mifereji ya maji machafu katika ya jiji,” aliongeza
Wakati huo huo, wadau kadhaa wa usombaji
taka katika jiji la Dar es Salaam wameomba serikali kutoa kipaumbele kwa
Dampo la Pugu Kinyamwezi na kulitengea bajeti ya kutosha ili liweze
kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment