Yusuph Mnyeto ‘Super Boy’ ‘Mtoto’ wa Kova aliyepania
kufuata nyayo za Rashid Matumla Na Michael Komba NDONDI ni miongoni mwa
michezo ambayo imewahi kuitangaza vilivyo Tanzania katika anga ya
kimataifa, kama ilivyokuwa kwa riadha. Mabondia ambao waliwahi
kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya
kimataifa, ni Michael Yombayomba, Habibu Kinyogori, Titus Simba,
Emmanuel Mlundwa, Rashid Matumla na wengineo. Soka ambayo ndio mchezo
unaopendwa na kupewa kipaumbele zaidi hapa nchini, haujawahi kuiletea
Tanzania mafanikio yoyote, zaidi ya kushiriki fainali za Kombe la
Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria. Zaidi ya mafanikio
hayo, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars na hata klabu zetu, zimebaki kuwa
‘kichwa cha mwendawazimu’ katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Angalau riadha na ndondi zimefurukuta kwa kutwaa medali katika
mashindano makubwa kama michezo ya Olimpiki na Michezo ya Afrika (All
Africa Games’. Pamoja na hilo, mchezo wa ndondi bado unaonekana kupewa
kisogo na wadau kwa kushindwa kuboresha miundombinu yake kama kumbu za
kisasa na mengineyo kama hayo. Hadi sasa, hakuna kumbi za kisasa za
mchezo huo hapa nchini ambazo zingesaidia kuwahamasisha vijana wadogo wa
kitanzania kujikita katika ndondi. Hatahivyo, bado kila siku ya Mungu
vijana wa kitanzania wameonekana ‘kupambana’ kujaribu kuendeleza vipaji
vyao kupitia ndondi, baadhi yao wakifanya hivyo bila kupata uangalizi
sahihi wa kitaalamu. Mathalani, katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar
es Salaam, unaweza kuwakuta vijana wadogo wakiwa wamening’iniza kiroba
kilichojaa mchanga juu ya mti, wakijifua waweze kutimiza ndoto zao za
kuwa mabondia maarufu hapa nchini na duniani kwa ujumla. Wapo wanaofanya
hivyo ili waweze kufikia mafanikio ya mabondia waliopita kama
Yombayomba, Simba; lakini wengi wakisikika wakimtaja Rashid Matumla,
ambaye ndiye bondia wa miaka ya hivi karibuni kuwahi kutamba hapa nchini
na hata katika medani ya kimataifa, akitwaa mikanda lukuki kabla ya
kustaafu. Yusuph Mnyeto ‘Super Boy’, ni miongoni mwa vijana wenye vipaji
vya ndondi ambaye ameona ni vyema akakitendea haki kipaji chake hicho.
Kijana huyo mwenyeji wa mkoani Tanga, ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi
chini ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiwa anapatikana pale
Polisi Ufundi, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, ni miongoni mwa
wachezaji wa timu ya ndondi ya Polisi jijini. Na baada ya kudumu katika
ndondi za ridhaa kwa muda mrefu kidogo, Mnyeto ameamua kubadili upepo na
kuhamia kwenye ndondi za kulipwa. Akizungumzia uamuzi wake wa kuhamia
ndondi za kulipwa, Mnyeto anasema kuwa alifanya hivyo kama sehemu ya
hatua za maisha yake katika mchezo huo aliodai kuwa anaupenda mno.
“Nimekuwa katika ngumi za ridhaa kwa muda mrefu, na sasa nimeamua
kuhamia ndondi za kulipwa, nikiamini ninaweza kupata mafanikio makubwa
kwani nina usongo wa kulipa sifa Jeshi la Polisi pamoja na nchi yangu
kwa kufanya mambo makubwa kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Katika maisha yangu ya ndondi, nimekuwa nikipata sapoti ya hali ya juu
kutoka kwa mwajiri wangu na wachezaji wenzangu ambao nao ni askari
Polisi… naondoka ngumi za ridhaa kwenda za kulipwa, nataka kurejesha
hadhi ya ndondi ndani ya Jeshi la Polisi. “Matarajio yangu ni kufuata
nyayo za Haji Matumla ambaye ni askari Polisi, Yombayomba (Michael) na
wenginbeo, ikiwezekana hata kuwazidi, naamini hilo linawezekana kama
kila kitu kitakwenda kama nilivyopanga.” Aliongeza: “Nataka kufanya kitu
tofauti, nashukuru hata rafiki na ndugu zangu, wananisapoti, sitaki
kubahatisha, ndio maana nimetafuta kocha mzuri mwenye uzoefu, kama
Rashind Matumla, ambaye nashukuru amenipokea na kunikaribisha katika
‘gym’ yake. “Kwangu Rashid Matumla ni mtu muhimu sana, nimekuwa
nikimshabikia tangu nilipokuwa mtoto na nilitamani siku moja nije kuwa
kama yeye au hata kumzidi. “Kufanya mazoezi katika ‘gym’ yake (Matumla),
kunanisisimua sana, ninapoona picha zilizopo katika ukuta wa gym yake
akiwa anapigana, akiwa amebeba mikanda mbalimbali ya ubingwa wa Dunia,
na hata habari za kwenye magazeti za kumpongeza, ninapata hisia kali
sana.” Anasema kuwa kikubwa zaidi, ni kuona bingwa huyo wa zamani wa
Dunia wa WBU ambaye alishiriki mara tatu michezo ya Olimpiki, mwaka
1988, 1992 na 1996, akimpa moyo wa kufuata nyayo zake “Kaka Rashid
amekuwa akinipa moyo kuwa kutokana na jinsi alivyoniona, ninaweza kuwa
bondia mzuri kama yeye au hata kumzidi, lakini kama nitafanya bidii
katika mazoezi, kuzingatia nidhamu na miiko ya mchezo huu wa ngumi.”
Mnyeto anaelezea hali ya ndondi ilivyo ndani ya Jeshi la Polisi,
akisema: “Polisi kuna wachezaji wazuri sana, tatizo ni hamasa, hivyo
nimeona ni vyema nikawafungulia njia wenzangu kwani hakuna sababu yoyote
ya kutofika mbali katika mchezo huo, maana mwajiri wetu anajali sana
michezo si kama katika sekta nyingine.” Kwa upande wa ndondi za ridhaa,
anasema kuwa tatizo lililoko huko ni uongozi wa chama husika kutokuwa na
mikakati ya kuuendeleza mchezo huo. “Katika ngumi za ridhaa hapa
nchini, tatizo ni uongozi, pale kuna mtu mmoja tu, Mashaga (Makore),
jamaa anajitahidi sana kupambana, kama angepata msaada, basi mambo
yangekuwa mazuri zaidi,” anasema. Na sasa Mnyeto ni ‘hakuna kulala’,
kila baada ya kumaliza majukumu yake ya kikazi, hugeukia mazoezi ya
ndondi katika gym ya Matumla na wakati mwingine kwenda kwenye klabu
nyingine za mazoezi. Katika mazoezi yake hayo, wakati fulani amekuwa pia
akinolewa na Haruna Andrew ‘Ndimu Mkata Shombo’ ambaye naye ni bondia.
Matarajio yake kwa siku chache zijazo ni kupata pambano la kujipima
nguvu dhidi ya bondia atakayejitokeza kukabiliana naye. “Kabla ya kupata
pambano, niliona ni vyema nikajifua kwanza kwani kuna kipindi
nilisimama kufanya mazoezi, hivyo lazima niwe fiti kabla ya kupanda
ulingoni,” anasema. Anasema kuwa matarajio yake mapema mwezi ujao
atakuwa fiti tayari kuonyesha ubabe na bondia yeyote atakayekubali
kupigana naye. Hata hivyo, alisema kuwa katika kufanikisha azma yake
hiyo, hatasita kuwa bega kwa bega na mwajiri wake ambaye ni Jeshi la
Polisi kuhakikisha kipaji chake hicho hakiathiri majukumu yake ambayo
ndiyo yanayomwezesha kufanikisha baadai ya mambo kuelekea mkakati wake
wa kuwa bondia hatari hapa nchini. “Pamoja na haya yote, ninaiheshimu
sana kazi yangu kwani ndiyo inayonifanya niwe na jeuri ya kutamba kutaka
kufuata nyayo za akina Matumla, bila Jeshi la Polisi, nisingekuwa kama
nilivyo sasa,” anasema Mnyeto. Bondia Yusuph Mnyeto, alizaliwa Februari
20, mwaka 1982 katika eneo la Ngamiani, jijini Tanga, akiwa ni mtoto w
asaba katika familia ya watoto saba wa Mzee Mnyeto. Alianza masomo yake
katika Shule ya Msambweni, jijini humo na baadaye kujiunga na Chuo cha
Ufundi Stadi (VETA) mwaka 1995.Mnyeto ambaye kwa sasa hajaona, lakini
akiwa na mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa muda si mrefu, alijiunga
na Jeshi la Polisi mwaka 2000 na hadi sasa analitumikia jeshi hilo, kwa
umakini na uadilifu wa hali ya juu. Pamoja na kulitumikia Jeshi la
Polisi na kuendeleza kipoaji chake cha ndondi, Mnyeto anekuwa akitenga
muda wake kwa ajilki ya kujiendeleza kimasomo. “Kama unavyofahamu, elimu
ni kila kitu na haina mwisho, nashukuru mwajiri wangu (Jeshi la
Polisi), hana kikwazo na mtu anayetaka kujiendeleza kimasomo, kwa kweli
ninashukuru sana kwa hilo,” anasema Mnyeto. Juu ya mkakati wake wa
kuendelea na masomo, anasema: “Ndondi inaonekana kama ni mchezo wa akina
‘Kayumba’ (watu wasio wasomi), tusikubali ujinga, mabondia twendeni
shule.” Kuhusiana na malengo yake baada ya kuanza kupata mafanikio
katika ndondi, anasema amepania kufungua klabu yake ya mazoezi ya ndondi
(gym) ambayo itakuwa katika ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana
chipukizi kujinoa waweze kutimiza ndoto zao. “Lengo langu ni kufungua
‘gym’ ambayo itakuwa na hadhi ya kimataifa, kama ilivyo Azam Complex ya
klabu ya soka ya Azam. Juu ya kilio cha mabondia wengi kutaka wadhamini
kujitokeza katika mchezo huo, Mnyeto anaasa: “Tusitegemee zaidi
wadhamini, tujitegemee, tusipigane kuganga njaa, kwani tunadhalilishwa
kwa kutojitambua, maana ukipigwa unajirudisha nyuma na umaarufu wako
unapotea.” tunamtakia kila la kheri Yusuph Mnyeto kuelekea
jitihada zake za kuwa bondia wa kulipwa mwenye mafanikio hapa nchini,
tukiamini hilo linawezekana iwapo atajipanga hasa na kuzingatia miiko ya
mchezo huo.
No comments:
Post a Comment