Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, March 19, 2015

MATUMLA AMPANIA KUMMALIZA MCHINAMwandishi Wetu
Wakati bondia Mohamed Matumla Jr akiwa katika mazoezi ya mwisho mwisho
kumkabili Wang Xin Hua wa China, wenzake Thomas Mashali na Karama
Nyilawila wametoleana uvivu huku kila mmoja akijigamba kutwaa ubingwa
watakapozichapa Machi 27 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar
es Salaam.
Matumla Jr atazichapa na Hua pambano la super bantam la ubingwa wa
dunia wa (WBF World Eliminate) pambano maalumu kwa mabondia hao la
kutafuta tiketi ya kucheza pambano la utangulizi kwenye lile la nguli
wa masumbwi duniani, Manny Pacquiao na Floyd Mayweather la Mei 2.
Kama Matumla atampiga Hua kwenye pambano lao la Machi 27 na kuonyesha
kiwango kizuri atapata nafasi ya  kucheza pambano la utangulizi
kuwasindikiza nguli hao wa masumbwi duniani watakapovaana Mei 2 jijini
Las Vegas.
Akizungumza katika mazoezi yake yanayoendelea kwenye gym ya Oil Com,
Keko jijini Dar es Salaam chini ya kocha wake ambaye ni baba yake
mzazi, Rashid 'Snake Man' Matumla, bondia huyo alisema hataki kupoteza
nafasi ya kucheza kwenye pambano la Mayweather na Pacquiao.
"Najua ugumu wa pambano langu na Hua hivyo sitaki kufanya mzaha, niko
fiti na sasa nafanya mazoezi mepesi ili kumkabili lakini pia sitaki
kupoteza nafasi ya kuwasindikiza nguli wa masumbwi duniani kwani ni
pambano ambalo 'litanitoa'," alisema Matumla Jr.
Kocha wake alisema, hivi sasa bondia huyo anajifua katika mazoezi ya
mwisho mwisho ambayo ni ya wepesi na kumweka tayari kumkabili Hua.
"Mudy yuko fiti, nimekuwa naye katika mazoezi, kiwango chake
kinaridhisha na sasa yuko katika hatua ya mwisho kabisa ambayo ni ya
mazoezi mepesi ya kumuweka tayari kwa pambano," alisema kocha wa
bondia huyo.

Promota wa pambano hilo, Jay Msangi alisema ili Matumla Jr apate
nafasi ya kuwasindikiza Pacquiao na Mayweather ni lazima aonyeshe
kiwango kwenye pambano lake na Hua.
"Tayari tumemwambia Matumla Jr vigezo hivyo kwani si ili mradi
kushinda bali aonyeshe kiwango kama ni ngumi ziwe ngumi kweli kwani
hawezi akacheza kwa kukumbatia na kushinda kwa pointi alafu apewe
nafasi ya kucheza Las Vegas, kule mashabiki wanataka waone ngumi hivyo
Matumla Jr anapaswa kupambana Machi 27 ili apate nafasi hiyo,"
alisema.
 
Siku hiyo pia, Japhet Kaseba atazichapa na Mada Maugo wakati Karama
Nyilawila akionyeshana ubabe na Thomas Mashali ambapo mabondia hao
kila mmoja amejigamba kutwaa ubingwa.
"Sina hofu na mpinzani wangu kwani kiwango chake nakijua na amekuwa
bondia wa kukimbia kimbia ulingoni hivyo ajiandae, cha msingi ni
mashabiki wangu kujitokeza kwa wingi kunipa sapoti," alisema
Nyilawila.
Wakati Mashali akijinadi kuwa yeye ataonyesha vitendo ulingoni siku
hiyo kwani nafasi ya kupigwa na Nyilawila haipo kwake na kusisitiza
kuwa yuko fiti na hatarajii kama mpinzani wake atamaliza raundi zote
siku hiyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...