DSC_0286
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Ltd Rhys Torrington akitia saini mkata wa kuonyesha Ligi Kuu ya Tanzania Bara moja kwa moja kupitia Azam TV. Katikati ni Makamu rais wa Shirikisho la Soka Tanzania  TFF Bw. Athuman Nyamiani.
DSC_0287
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Ltd Rhys Torrington (kulia) na Makamu wa rais wa TFF Athuman Nyamiani baada ya kutiliana saini mkataba huo.
Kampuni ya Azam Media sambamba na Shirikisho la Soka Tanzania TFF zimetiliana saini mkataba wa kuonyesha mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara moja kwa moja katika msimu huu wa 2013/2014.
Kampuni hiyo ya Azam imesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuonyesha mechi hizo kupitia Azam TV wenye thamani ya shilingi 5,560,800,000/= ambao utalipwa kwa awamu tatu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Makamu Rais wa TFF Bw. Athuman Nyamiani amesema Shirikisho la Soka limefurahi kushirikiana na Azam Media na kuwa hatua hiyo ya kuonyeshwa kwa mechi hizo itazisaidia klabu kujitangaza na kupata wadhamini wa ndani na nje ambako Azam TV itakuwa ikionekana.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Ltd Rhys Torrington amesema king’amuzi cha Azam TV kitaanza kupatikana hivi karibuni kwa bei nafuu na kitakuwa na chaneli zaidi ya 50 huku ligi kuu ikiwa moja wapo.
Ameongeza kuwa ni lengo la kampuni ya Azam Media Ltd kulifanya soka la Tanzania kujulikana na kuwa maarufu barani Afrika na kimataifa kwa ujumla.