Kocha mpya wa Ashanti United, Hassan Banyai (kulia)
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Moro United, Hassan Banyai,
ameteuliwa kuchukua mikoba ya Hassan Mubaraka 'Muba' wa Ashanti United baada ya
kocha huyo kukosa sifa za kufundisha Ligi Kuu Bara, na ameapa kuendeleza makali
ya timu hiyo.
Muba ambaye alijiwekea rekodi mpya baada ya
kuipandisha timu hiyo kwa mara ya pili Ligi Kuu, ameshindwa kuendelea kuinoa
timu hiyo baada ya kutotimiza vigezo vya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu
Tanzania (TAFCA).
Kwa mujibu wa taratibu za TAFCA, kocha anayepaswa
kufundisha Ligi Kuu ni yule mwenye cheti kuanzia ngazi ya Kati (Intermidiate
Course).
Akizungumza na Nyumba ya Michezo na Burudani, Katibu
Mkuu wa Ashanti United, Abubakari Silas, alisema baada ya TAFCA kutoa angalizo hilo wameona ni
bora wakajipanga mapema ili kuepuka usumbufu watakaoupata baadaye
"Baada ya uongozi kushauriana kwa kina na
kugundua kwamba kocha tuliyenaye hajakidhi viwango vya TAFCA licha ya kuwa na
uwezo mkubwa wa kufundisha, ndio maana tukaamua kumchukua Hassan Banyai,"
alisema.
Alisema wanamuheshimu Muba na wataendelea kumthamini
kwa kazi kubwa aliyoifanyia timu hiyo na wana imani hiyo ni changamoto kwake
atakayoichukulia katika mtazamo mzuri zaidi wa kimaendeleo.
Mbali na hilo, Silas alisema pia wamekubaliana Rais
wa timu hiyo wa sasa, Msafiri Mgoyi, aendelee kuwa katika nafasi hiyo akisaidiwa
na Almasi Kasongo katika umakamu rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).
Akizungumzia zaidi timu yao iliyoko nchini Burundi
kujiwinda na ligi kuu, alisema inaendelea vizuri na kwamba imecheza mechi moja
na timu ya daraja la kwanza nchini na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Alisema bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wao
ambaye pia ni mshauri wa benchi la ufundi, Said Maulid 'SMG' katika mchezo
walioonesha kiwango kizuri na wanatarajia kurudi jijini Ijumaa.
Kwa upande wake, Banyai ametamba kuipa mafanikio timu hiyo na kuwaahidi mashabiki wa Ashanti kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya timu hiyo.
No comments:
Post a Comment