Feza akihojiwa na IK siku alipotolewa BBA
Feza Kessy
Na Andrew Chale
“UTAMADUNI wa Kitanzania
umenisaidia kuiwakilisha vyema nchi yangu kwenye shindano la Big Brother Africa
‘The Chase’ na kujifunza mengi pia”, hiyo ni kauli ya Feza Kessy wakati wa akijibu
maswali ya wandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Feza aliyetua nchini juzi
jioni akitokea Afrika Kusini kwenye shindano hilo, ametolewa zikiwa zimebaki
siku 14 kumalizika, ambako hivi sasa washiriki saba pekee wamebaki ndani ya
Jumba kuchuana ili kuondoka na kitita cha dola 300,000 za Kimarekani,
Anasema, utamaduni huo wa
Kitanzania uliomfanya kuweza kukaa kwa siku 77 ndani ya jumba hilo, umeweza
kumfanya ajisikie Mtanzania mwenye bahati, kwani aliweza kuvumilia mambo mengi
kutoka kwa washiriki wenzake waliotoka nchi zaidi ya 14 barani Afrika, wenye
tamaduni tofauti.
Akiendelea kujibu maswali ya
wandishi, Feza anakiri kuwa na uhusiano na
Oneal, mshiriki kutoka Botswana, ambaye naye alitolewa wiki moja kabla
ya Feza.
“Ni kweli nilikuwa na mahusiano
ya kweli na Oneal nilipokuwa ndani ya jumba la Big Brother, zaidi ya hapo ni
shindano tu,” anasema Feza.
Hata hivyo, alipoulizwa kama
wataendelea na uhusiano nje ya hapo, Feza anasema, ni mapema mno kujibu hilo,
kwani amepanga kutulia, kujadili kwa kina suala hilo na kisha atachukua uamuzi.
“Oneal yupo Botswana na mimi
nipo Tanzania, sote kwa pamoja hatuna la kusema ila kila mtu anajipanga na
litakalotokea tutatoa taarifa,” anasema
Feza na kuongeza.
Anashukuru kwa kuwa
mwakilishi wa Tanzania ndani ya shindano hilo na kujiona mtu mwenye bahati.
“Kwanza nashukuru Mungu
kuchaguliwa kwangu ndani ya jumba la Big Brother, licha ya kujitokeza wengi
mimi ni miongoni mwa washindi, hivyo namshukuru Mungu,” anasema.
Akitoa ushauri kwa vijana,
Feza anawataka wasivunjike moyo, zaidi wajitume ili kupambana na maisha ya kila
siku na watafikia pale wanapopataka.
MAISHA NDANI YA
BBA
Tanzania awali iliingiza
washiriki wawili ndani ya jumba hilo, akiwamo Nando aliyetolewa kwa utovu wa nidhamu na
kumuacha Feza ambaye hadi anatolewa alikaa siku 77 pekee.
Kukaa kwake ndani ya jumba
hilo, Feza aliweza kuhimili mambo mbalimbali, ikiwemo michezo na kazi
zilizokuwa zikitolewa na mkuu wa jumba hilo, Bigg.
Pia, Feza aliwahi kukwaruzana
na mshiriki mwenzake, Pokelo wa Zimbabwe
na kusema kuwa, ilikuwa ni sehemu ya mchezo, kwani kila mmoja alikuwa na mambo
sawa ya kufanana.
“Sikuchukiana na Pokelo,
ukiwa ndani ya jumba lile ni mchezo, kwani mimi na yeye sote tunashabihiana mambo
yetu, ikiwemo tarehe za kuzaliwa na sote kwa pamoja tuna mtoto,” anasema Feza.
FEZA AMETOKEA
WAPI?
Feza, awali alikuwa
mlimbwende na kutwaa taji la Miss Dar City Centre na Miss Ilala mwaka 2005.
Licha ya urembo, pia aliingia rasmi kwenye muziki huku akikiri kupenda muziki hata kabla ya
kushiriki shindano la Miss Tanzania.
Feza anasema, alizaliwa
mkoani Arusha miaka 25 iliyopita na kupa elimu yake nchini na kisha Uingereza
katika mji wa Manchester, ambako pia alipata mtoto wa kiume.
Wimbo wake aliyoutoa awali,
aliutoa kwa kushirikiana na msanii Nash, ukienda kwa jina la ‘Strong Woman’.
Feza anasema, anawakubali
wasanii mbalimbali nchini, wakiwemo Mwana FA, TID, marehemu Ngwair, Nurah, Ommy Dimpoz na AY
huku ndoto zake kubwa katika muziki ni kufanya kazi kwa pamoja na Rihanna,
Lauryn Hill, Tony Braxton na wengine pindi akipata nafasi.
Imeandaliwa na
Andrew Chale 0688076376
No comments:
Post a Comment