Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, December 10, 2012

JOKHA KASSIM Mwimbaji wa taarabu anayetamba na T-Moto


Jokha Kassim
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIPATA bahati ya kuusikia wimbo wa Riziki Mafungu Saba, hakika utaanza kuupenda muziki wa taarabu, hata kama awali hujaupenda.
 
Ni wimbo mzuri. Wenye mashairi mazito na yenye ujumbe murua, unaoelezea jinsi riziki zinavyopangwa na Mungu na wala sio binadamu, wakiwamo wenye roho mbaya.
 
Wimbo huo umeimbwa na mwanamama Jokha Kassim, alipokuwa na kundi zima la Zanzibar Stars Modern Taarab.
 
Kwa sasa Jokha anafanya kazi katika kundi zima la Tanzania Moto Modern Taarab, maarufu kama T-Moto, lenye wakali wengine kibao.
 
Tayari Jokha amerekodi wimbo unaokwenda kwa jina la ‘Domo la Udaku’, ukiwa ni ujio mpya wa kundi hilo la taarabu nchini.
 
Mwimbaji huyo juzi alifanya mazungumzo na Fiesta Magazine na kusema kuwa muziki ni kipaji chake, alichobarikiwa na Mungu.
 
Cheche zake zilianza kuonekana tangu zamani, alipokuwa hodari sana wa kuimba nyimbo mbalimbali za taarabu.
 
“Muziki huu ni kipaji changu, tangu zamani niliweza kuimba kwa ufanisi na kushangaza wengi waliokuwa wakiona mahala popote.
 
“Nashukuru, leo hii nimeweza kufanya juhudi na kufika T-Moto, ikiwa ni baada ya kujulikana nilipofanya kazi na Zanzibar Stars kwa mafanikio makubwa,” alisema.
 
Licha ya kuanza zamani kuimba, lakini alianza kuingia kwenye kundi la muziki mwaka 2002, alipohitajiwa na uongozi wa Zanzibar Stars na kumtambulisha kimuziki.
 
Kilichomkwamisha kuingia mapema kwenye sanaa ni kukatazwa na wazazi wake, hivyo kusubiri hadi mwaka huo alipoanza kushika kipaza sauti na kurindimisha sauti yake.
 
Jokha alikuwa mke wa kwanza wa Mfalme, Mzee Yusuph, ila kwa sasa wameachana na kila mmoja anaishi kivyake.
 
Siku chache baada ya kuachana na mzee Yusuph, hamu ya kuimba ilimtesa, hivyo kuamua kufanya harakati za kuibua kipaji chake.
 
Jokha na Mzee Yusuph wamezaa mtoto mmoja, ambaye pia ni mwimbaji na Mkurugenzi wa kundi la Jahazi Modern Taarab.
 
“Nilifanya kazi ya ziada kuingia kwenye muziki, maana baba yangu hakupenda suala hilo, hivyo kunipa wakati mgumu.
 
“Hata hivyo Mungu akipanga lake hakuna wa kuweza kutengua, ndio maana nimeweza kufika hatua hii na kujulikana sehemu kubwa kupitia soko la muziki wa taarabu,” alisema.
 
Mwimbaji huyo mwenye mvuto wa aina yake, anashindwa kubainisha chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake na mume wake Mzee Yusuph.
 
Anasema riziki imekwisha kwa ndoa yao, huku akisema bado wanaheshimiana kwasababu wameachana bila kuwa na ugomvi, huku wakifanikiwa kupata mtoto mmoja, aliyepewa jina la Yusuph Mzee Yusuph.
 
Muziki wa taarabu unazidi kufanya vizuri kutokana na waimbaji wake wengi kuwa wabunifu.
 
Katika hilo anaamini kuwa mambo yatazidi kuwa mazuri, huku mashabiki wakipata vitu adimu kutoka kwao.
 
Mwimbaji huyo anavutiwa na mkali wa muziki huo nchini, Zuhura Shaaban.
 
Katika kundi lake la T-Moto, Jokha ameimba nyimbo zaidi ya tatu, ukiwamo wa ‘Unavyojidhani Haufanani’ ‘Mimi ni Star’ na ‘Aliyeniumba Hajanikosea’, ambao ulibeba jina la albamu ya kwanza.
 
Kwa albamu hii mpya inayoandaliwa, Jokha amesharekodi wimbo mmoja unaokwenda kwa jina la Domo la Udaku.
 
Katika hilo, ni wazi kuwa wao watakuwa juu zaidi, maana bendi nyingi zimekosa ubunifu na mikakati ya kimuziki.
 
“Kwenye muziki kumekuwa na ushindani, hivyo nadhani kinachotakiwa ni mipango, mikakati pamoja na nyimbo nzuri.
 
“Sisi tunavyo vitu hivyo, nadhani ni wakati wetu kuwa kileleni maana mashabiki wana kiu ya kuona mambo yetu yanakuwa mazuri,” alisema.
 
Jokha alizaliwa miaka kadhaa iliyopita, Zanzibar, katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
 
Elimu ya Msingi aliipata katika shule ya Darajani na kuhitimu mwaka 1995 ile ya Sekondari aliipata kwenye shule ya Haile Selasi.
 
Mbali na Jokha, wengine wanaopatikana kwenye kundi hilo ni pamoja na Nyawana Fundikira, Aisha Masanja, Shimuna Kassim, Amina Rashid, Hanifa Juma, Shaban Ramadhan, Mrisho Rajabu, Rahma Omari, Silver Mwandilee, Kasikile Msukule na wengineo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...