Na Mwandshi Wetu
BAADA ya makamuzi aliyoyafanya wiki iliyopita kwenye ukumbi wa
Garden Breeze, mkali wa muziki wa dansi nchini, Ali Choki ‘Mzee wa Kibaha,'
Jumapili hii atarejea tena katika viunga hivyo vilivyoko Magomeni Mapipa jijini
Dar es Salaam kuwakimbiza.
Choki akiwa na bendi yake ya Extra Bongo Next Level, ‘Wazee wa
Kizigo’ sambamba na mkali mwingine wa muziki huo nchini, Ramadhani Masanja
‘Banza Stone’, alidihirisha uwezo wake mkubwa wa uimbaji na kukonga vema nyoyo
za mashabiki waliomba marejeo hayo.
Akizungumzia shoo ya Jumapili hii, Choki alisema, bendi yake
imepania kuhakikisha inakonga nyoyo za mashabiki wao wa Magomeni na maeneo ya
jirani na kwamba, kila atakayehudhuria atakubaliana na hilo.
“Kazi zetu zinatambulika, watakaokuja watashuhudia shoo kali
kutoka kwa wanamuziki na wanenguaji mahiri wa dansi. Waje kwa wingi na kila
atakayeingia Garden Breeze, hatojutia uamuzi wake wa kuja kujinafasi nasi wana
wa ‘Next Level’ wikiendi hii,” alitamba Choki.
Aidha, mkongwe wa dansi Afrika Mashariki na Kati, Tshimanga Kalala
Asosa, naye atafanya vitu adimu akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz,
watakapotumbuiza kwenye ‘kijiji hicho cha maraha’ cha Garden Breeze leo usiku.
Asosa maarufu kama ‘Mtoto Mzuri’, alisema, amejiandaa kukonga
nyoyo za mashabiki kwa vibao vyake vipya na vya zamani, vikiwamo vile
vilivyompa umaarufu mkubwa, kiasi cha kuitwa hapa nchini kuanzisha bendi kongwe
ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ mwaka 1978.
No comments:
Post a Comment