Jirani
wa nyumba no:-497 iliyoungua moto katika mtaa wa Baghani Mjini
Zanzibar Bi.Salma Haroub, aliyeshuhudia tukio hilo akimpatia maelezo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika eneo
hilo kuifariji familia ya Bibi Farida Abdulla iliyopatwa na mkasa huo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia baadhi ya
sehemu zilizoathiriwa na moto ndani ya nyumba ya Familia ya Bibi Farida
Abdulla iliyopo Mtaa wa Baghani Mjini Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua warsha ya
siku mbili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati za Uongozi na
menejimenti za Tasaf Zanzibar juu ya mpango wa Taifa wa kunusuru kaya
maskini.
Mbunge
wa Jimbo la Kiembe Samaki Mh. Waride Bakari Jabu na Mbunge wa Viti
Maalum Dr. Maua Abeid Daftari wakiwa miongoni mwa wajumbe wa kamati za
uongozi na menejimenti za Tasaf Zanzibar kwenye warsha yao ya siku mbili
inayofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya
pamoja na Uongozi wa Juu wa Tasaf pamoja na Wajumbe wa Kamati za Uongozi
na Menejimenti za Tasaf Zanzibar nje ya ukumbi wa Zanzibar Beach Resort
Mbweni mara baada ya kuifungua warsha yao ya siku mbili. Hassan Issa – Mpiga picha – OMPR-ZNZ
*********************************
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imethibitisha azma yake ya kuunga mkono
utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kunusuru kaya maskini katika Shehia
mbali mbali hapa Zanzibar ili kuondoa umaskini kwa manufaa ya Jamii na
Taifa kwa ujumla.
Mpango
huo uliomo ndani ya awamu ya Tatu ya mfuko wa maendeleo ya Jamii
Tanzania { Tasaf } unatarajiwa kuwafikia walengwa wapatao milioni moja
na Laki Tano Tanzania Bara na Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati
akifungua warsha ya siku mbili ya kujenga uelewa wa mpango wa Taifa wa
kunusuru kaya maskini kwa wajumbe wa Kamati za Uongozi na Menejimenti za
Tasaf hapo katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya
Mji wa Zanzibar.
Balozi
Seif alisema kwamba ili malengo ya mpango huo yafikiwe na kufanikiwa
ipasavyo ushiriki wa wadau mbali mbali unahitajika katika kujizatiti
kutekeleza miongozo na taratibu ndani ya maeneo kwa ufanisi mkubwa.
Alifahamisha
kwamba kaya zitakazohusika na mpango huo zitafaidika kwa kushiriki
mpango wa Jamii wa Uhawilishaji Fedha, Miradi ya ujenzi itayotoa ajira
ya muda, miradi ya ujenzi kwa kutoa huduma za Elimu, Afya na Maji pamoja
na shughuli za kuweka akiba pamoja na kuwekeza na kujengewa uwezo.
Alielezea
matumaini yake kwamba mpango huu wa kunusuru kaya maskini utaimarisha
uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa makundi mbali mbali kushiriki kwa
kutumia mfumo madhubuti wa kubaini walengwa ndani ya shehia mbali mbali.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza na kuwashukuru washirika wa
maendeleo wa Uingereza, Marekani wakiongozwa na Benki ya Dunia { World
Bank } kwa kukubali kuchangia mpango huo.
Akitoa
tathmini ya miradi ya Tasaf awamu ya Pili kwa upande wa Zanzibar Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salim Moh’d
alisema jumla ya miradi 820 ya maendeleo imetekelezwa ndani ya awamu
hiyo ikigharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 12.
Dr.
Khalid alizipongeza Kamati tofauti za Uongozi za Tasaf katika wilaya
na shehia mbali mbali za Zanzibar zilizopelekea ufanikishaji mkubwa wa
utekelezaji wa awamu ya Pili ya mradi wa Tasaf.
Hata
hivyo Dr. Khalid alizitaja baadhi ya changamoto zilizoleta matatizo
ndani ya utekelezaji huo ambazo ni pamoja na soko la bidhaa za wajasiri
amali, Taaluma iliyochangia kutokukamilika baadhi ya miradi pamoja na
uwajibikaji mdogo kwa baadhi ya Taasisi ulioshindwa kuratibu vyema awamu
ya Pili.
Mapema
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Bwana
Ladislaus Mwamanga alisema dhana ya Mfuko huo katika kupunguza umaskini
Nchini ndani ya kipindi cha miaka 12 tokea kuanzishwa kwake haikufikiwa
kama ilivyokusudiwa.
Bwana
Mwamanga alisema Tasaf awamu ya Tatu inalenga kuwajengea uwezo zaidi
watendaji watakaosimamia mpango huo ili kuwafikia walengwa ambao ni
Wananchi pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto zote zilizoibuka ndani
ya awamu ya Pili ya Tasaf.
Mapema
asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika
Mtaa wa Baghani Mjini Zanzibar kuifariji Familia ya Bibi Farida Abdulla
ambayo ilipata hasara baada ya nyumba wanayoishi kuungua Moto.
Nyumba
hiyo iliyo chini ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya amana Zanzibar yenye
nambari za usajili 497 iliungua sehemu ya juu ambapo mmoja wa majirani
walioshuhudia moto huo Bibi Salma Haroub alimueleza Balozi Seif kwamba
chanzo cha moto huo wanafikiria huenda ikawa hitilafu za Umeme.
Bibi
Salma alisema kizaa zaa hicho kilisababisha majirani waanze kuchukuwa
hatua za kukabiliana na moto huo na baadaye kusaidiwa na Kikosi cha zima
moto na uokozi wakifanikiwa kuwaondoa Watoto wawili waliokuwemo ndani
ya nyumba hiyo ambapo mzazi wao hakuwepo wakati wa tukio hilo.
Kiongozi
Mmoja wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Bwana Abdulla Haji Steni
alielezea kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya wateja wa huduma hiyo
kuamuwa kuongeza vifaa tofauti vya umeme bila ya kutoa Taarifa kwenye
shirika na wakati mwengine kusababisha hitilafu zinazozaa maafa.
Akitoa
nasaha zake mara baada ya baadhi ya wakaazi wa eneo hilo la tukio kutoa
shutuma kwa wahandisi wa Shirika la Umeme watati linapotokea tatizo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa
shirika hilo kuchukuwa hatua za haraka wakati wanaporipotia kutokea kwa
hitilafu za umeme.
Balozi
Seif alisema zipo kumbu kumbu za matukio kadhaa ya hitilafu za umeme
yanayojitokeza na kuripotiwa kwa wahandisi wa shirika hilo lakini
utekelezaji wake huchukuwa muda mrefu na kuleta hali ya wasi wasi wa
wananachi katika maeneo hayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/1/2013.
No comments:
Post a Comment