Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, January 15, 2013

Wajawazito Wamuomba Mengi awasaidie wasijifungulie njiani


Watoto wa kitongoji cha Ifumbo Wilaya ya Mvomero wakipeleka maji na chakula kwa vijana waliokuwa wakichimba kutengeneza barabara kwa kutumia majembe ya mkono kama walivyokutwa na kamera ya BRYCESON NYEREGETE.


 Na Bryceson Mathias, Mvomero
 
WAKATI Serikali ya Kata ya Mvomerowilayani humo ikiwa bado inatafakari kuwasaidia wananchi wa Ifumbo kupata barabara ili wajawazito wanaojifungulia njia wawahi kufika kwenye zahanati iliyoko kilomita 10, akina mama 31 waliojifungulia njiani akiwemo aliyejifungulia chini ya mwembe Selina Jovini, wamemuomba Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi awasaidie kero yao.
 
Hayo yalisemwa hivi karibuni na akina Mama Wakazi wa Kitongozi cha Ifumbo wilayani humo, ikiwa ni mara tu baada ya kuwapelekeaa Maji ya Kunywa na Chakula Vijana na waume waliokuwa wakichimba Barabara kwa majembe ya Mkono ili kuwanusuru wake zao waondokane  na adha hiyo.
 
Akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi  Selina Jovini, ambaye Mwaka Jana alijifungua mtoto wa kike chini ya mti wa mwembe baada ya kubebwa umbali wa kilomita 10 na watu wakiwemo wazazi wake kufuata zahanati iliyoko Mvomero mjini kutokana na ukosefu wa barabara alisema,
 
“Tunamsikia tu Dkt. Mengi kwenye Radio tunazofungua huku kwetu milimani kusiko na barabara wala TV, kwamba anawasaidia sana akina mama, watoto na walemavu sehemu mbalimbali, tunamuomba Baba huyu mwenye utu aje na kwetu tunakojifungulia chini ya miembe baada ya kubebwa minzeganzega, ili atunusuru na vifo”.alisema Selina Jovini.
 
Selina Jovini ambaye Baba yake ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji hicho kwa tiketi Chama cha Mapinduzi (CCM) alijifungua chini ya mti huo baada ya Baba yake Bw. Jovini Victor (54) akisaidiana na wasamari wema kumbeba kwa umbali wa Kilomita Sita wakibakiwa na Nne ili wafike ilipo Zahanati, na kukiri kuwa  tukio hilo liliwatokea saa 10 usiku Desemba 23, 2012.
 
Akilikumbuka tukio hilo Victor alisema, siku hiyo baada ya kuvuka mabonde, milima na mito miwili mwanae alimuomba mama yake mzazi wazungumze pembeni chini ya mti wa mwembe,  ambapo alidai kwa haraka alibaini kuna jambo limeharibika na kuwaachia nafasi, na baada ya muda mfupi alisikia sauti ya mjukuu wa kike chini ya mwembe huo ikilia.

Victor ambaye wakati huo alikuwa anatoka kumpeleka mkewe Hosipitali Misheni ya Bwagala kutibiwa ambayo iko kilomita zaidi ya 50 toka Kitongoji cha Ifumbo alisema, Kero ya Barabara kwenye eneo lake bado haijatatuliwa na wananchi wake wataendelea kupata matatizo hayo na ikibdidi vifo, kutokana na kukosekana anayewajali ingawa eneo hilo lina rasilimali ya madini.
 
Aidha Diwani wa Viti Maalum wa Juliana Petro (CHADEMA) alisema, Kero hiyo inamkera sana Moyoni mwake mbali ya kumnyima usingizi na hadi sasa anaumiza kichwa chake kuona ni jinsi gani akina mama wa eneo hilo watakombolewa na adha ya Barabara ambayo waume zao wanaendelea kung’ang’ana kuichimba bila mafanikio, lakini alipenda serikali wilayani ikubali mawazo ya wananchi kutaka barabara fupi badala ya ile ya mzunguko ambayo wanaifikilia.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...