Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando (kulia) na Makamu wake, George John.
****************************************************
CHAMA
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimepanga kufanyika
mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) Februari 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Uamuzi
wa kuendesha mdahalo huo ulifikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji
ya TASWA kilichofanyika jana (Januari 23, 2012), ambapo pia kilijadili
masuala mbalimbali yahusiyo chama hicho.
Tayari kikao kimeiagiza
Sekreterieti ya TASWA ifanye maandalizi ya mdahalo huo kwa kuzungumza na
vituo vya televisheni ili uweze kuoneshwa moja kwa moja kwenye vituo
hivyo ili wananchi waweze kuwasikia wagombea hao.
Pia mazungumzo ya awali na
wadhamini mbalimbali yameanza kuweza kufanikisha tukio hilo la kuendesha
mdahalo wa 'live' kwenye televisheni. Nafasi ambazo wahusika
watafanyiwa mdahalo ni Rais na Makamu wa Rais.
TASWA imekuwa ikifanya mdahalo
kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo
mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka
2008, ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa, hivyo itafanya
mawasiliano na TFF ili iweze kupata msaada wa karibu kufanikisha jambo
hilo.
Tunaamini ushirikiano uliopo
kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha jambo hilo,
ambapo mdahalo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa michezo,
wahariri wa baadhi ya michezo na wadau wachache wa soka.
Kutokana na hali hiyo Kamati
ya Utendaji ya TASWA imemteua mwandishi wa habari mkongwe ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Redio ABM, Abdallah Majura kuwa mwendeshaji wa
mdahalo huo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya habari na mambo ya
michezo.TASWA inaamini Majura ambaye ni mwanachama wa TASWA akiwa pia
amepata kuwa Katibu wa TASWA FC na Mhazini wa TASWA ni mtu makini,
asiyeyumba na mwenye kutenda haki.
Pia Kamati ya Utendaji
imesisitiza katika kikao chake kwamba uchaguzi wa TFF haimuungi mkono
mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote, hivyo
TASWA inaonya kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia
mgongo wa TASWA kwamba chama kinawaunga mkono ili wapate mteremko
kufikia malengo yao hazitatimia.
Kama kuna kiongozi au
mwanachama wa TASWA ambaye anamuunga mkono mgombea yeyote wa TFF, huo
utakuwa msimamo wake binafsi si wa chama na kama atahusisha chama kwa
namna yoyote atakuwa anakosea na hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa
mujibu wa katiba ya chama.
Tunawaomba waandishi wa habari
za michezo nchini kuzidisha umakini kipindi hiki cha uchaguzi wa TFF na
kujiepusha na makundi ya aina yoyote ambayo yatatia doa taaluma ya
habari kwa namna yoyote ile.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
24/01/2012
No comments:
Post a Comment