Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, January 16, 2013

19 WACHUKUA FOMU TFF


WADAU 19 wa soka nchini wamechukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), unaotarajiwa kufanyika Februari 24, mwaka huu.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wadau wawili wameomba kugombea nafasi ya makamu wa rais wakati wengine 17 wameomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wambura aliwataja waliochukua fomu za kuwania umakamu wa rais kuwa ni Wallace Karia na Ramadhan Nassib, ambao kwa sasa ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda wake.

Aliwataja waliochukua fomu za ujumbe kuwa ni Shaffih Dauda, Athuman Kambi, Hussein Mwamba, Stewart Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona, Vedastus Lufano, Twahili Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi, Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James Mhagama na Selemani Bandiho.

Ada kwa wagombea wa nafasi ya urais ni sh. 500,000, makamu wa rais sh. 300,000 na wajumbe wa kamati ya utendaji sh. 200,000.

Wagombea katika uchaguzi huo, wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania, kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne, uzoefu wa uendeshaji wa soka, wasiwe na hatia ya makosa ya jinai na umri usiopungua miaka 25.

Pia wanatakiwa wawe wamewahi kucheza soka, waamuzi, makocha au kuendesha soka katika ngazi yeyote wakati kwa nafasi ya urais na makamu wa rais, wagombea wanatakiwa kuwa na shahada ya chuo kikuu na uwezo wa kuwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...