DAR ES SALAAM, Tanzania
MAALIM Hassan Yahya Hussein, amepinga kauli
iliyotolewa hivi karibuni na mtabiri mwenzake kuwa rais wa mwaka 2015 kuwa
atakuwa mwanamke.
Akizungumza na
wandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu utabiri wake wa
matukio yatakayotokea mwaka 2013, ambapo mwaka huo utaanza Machi 21
mwaka huu.
Maalim Hussein alisema kiutabiri huwezi kutoa utabiri
katika matukio ya mwaka mmoja mbele, kitendo cha mtabiri huyo ni sawa na
kuwakatisha tamaa baadhi ya watu wenye nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo mwaka
2015.
“Huwezi kutoa utabiri wa miaka miwili mbele hata
Sheikh Yahya Hussein mtabiri aliyekuwa akikubalika hakuwahi kufanya hivyo, pia
sikubaliani naye kuwa rais ajaye atakuwa mwanamke hata ukiangalia katika njia
zetu za utabiri ambazo ni namba zinapingana na hilo”alisema.
Alisema matokeo ya utabiri kama huo ni sawa na
uwamuzi wa kuwafungia milango kidemokrasia baadhi ya wanasiasa wenye nia ya
kugombea urais mwaka 2015.
“Kuna baadhi ya viongozi wakiwemo Lowassa na Membe
wanadaiwa kuwa huenda wakagombea nafasi hiyo, kwa kufanya hivyo itakuwa ni
kuwakatisha tamaa”alisema.
Akizungumzia utabiri wa mwaka huu, alisema kuwa kuna
viongozi wengi, wabunge, wakuu wa mikoa na wengine watatoa matamshi ya utatanishi na kusababisha hofu na mitafaruku
itakayowafanya watu kupigana.
Vile vile
alisema wapo wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataungana
katika masuala ya msingi yatakayohusu utaifa bila kujali itikadi zao za kivyama
au kimajimbo.
Maalim Hussein alibainisha kuwa Rais Jakaya Kikwete
ataunganisha nchi na kuwa moja yenye uimara wa utaifa kuliko watangulizi wake,
akishirikiana zaidi na wanasiasa na viongozi wa dini kuondoa mtikisiko wa
uvunjifu wa amani uliyojitokea mwaka jana.
Aidha, Chama kimoja cha siasa kitajitokeza na
kitachochea kujitenga na kuunda Taifa lake hata hivyo, kusudio hilo
halitafanikiwa kwani litapingwa na Watanzania wote kwa kauli moja na vitendo.
Maalim Hussein pia alisema kutatokea vifo vya ghafla
kwa watunzi wa hadithi na vitabu, wandishi wa habari, wanasiasa na wasanii
ambapo matukio hayo yatakuwa mabaya zaidi kuliko mwaka jana.
Akigusia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika hivi
karibuni nchini Kenya ambao ni
majirani, alisema kuwa Muungano wa CORD, ukiongozwa na Raila Odinga utashinda
uchaguzi huo, ambao ana amini utakuwa wa amani na tulivu.
“Ushindi huo utakuja baada ya kuushinda Muungano wa
Jubilee ukiongozwa na akina Uhuru Kenyata na Ruto pamoja na ule wa Musalia
Mudavadi unaoitwa AMANI”alisema.
No comments:
Post a Comment