Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, March 27, 2013

Simba chali Kaitaba, Azam ikitakata Dar



WAKATI wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa, Azam wakitaka jijini Dar kwa kuigaragaza Prisona ya Mbeya kwa mabao 3-0, mabingwa watetezi Simba wamejikuta wakiangukia pua mjini Kagera baada ya kudunguliwa bao 1-0 na wenyeji wao Kagera Sugar.
Azam walipata ushindi huo kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi, na kuweza kupunguza pengo la pointi kati yao na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanaoongoza wakiwa na pointi 48.
Mabao mawili na kinara wa ufungaji bora kwa sasa Kipre Tchetche na moja ya John Bocco 'Adebayor' yalifanya Azam ikifikishe pointi 40 na kuweka matumaini ya kuikamata Yanga ambayo haikushuka dimbani leo.
Bao la kwanza la Azam lilifungwa na Kipre katika kipindi cha kwanza kabla ya Bocco kuongeza la pili kipindi cha pili na Kipre kuongeza bao la tatu dakika za jioni na kuifanya Azam kutakata kabla ya kuvaana na Barrack YCII watakaorudiana nao katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika siku ya Jumamosi.
Wakati Azam wakimeremeta Dar, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Simba yenyewe walikiona cha mtema kuni baada ya kulambwa bao 1-0 na Kagrea Sugar katika pambano jingine lililochezwa uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Bao la sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili lililofungwa kwa kichwa na beki Amandus Nesta akiiunganisha kona ya Salum Kanoni iliifanya Kagera kufika pointi 34 sawa na Simba.
Hata hivyo Kagera imekamata nafasi ya nne kutokana na kuzidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na Simba ambao wamezidi kuwasononesha mashabiki wao ambao wamekuwa hawana raha kwa timu yao kuwa na matokeo mabaya msimu huu tofauti na matarajio yao.
Ushindi huo wa Kagera imekuwa muendelezo wa kuvinjuka 'vigogo' kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani hata Yanga walipoenda mjini humo walipigwa bao 1-0 na kuibua tafrani kwa waandishi wa habari waliotuhumiwa kuhujumu pambano hilo.
Kagera mbali na kuikamata Simba kiponti pia imeziengua timu za Mtibwa Sugar na Coastal Union ambazo sasa zimeporomoka katika nafasi walizokuwa wakizishikilia hadi nafasi ya tano na sita badala ya zile za nne na tano walizokuwa wakishikilia awali.
Baada ya kipigo hicho Simba inatarajiwa kusafiri mpaka jijini Mwanza kuvaana na timu ya Toto Africans ambayo huwa inawasumbua kwenye dimba la CCM Kirumba.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...