Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, March 27, 2013

SIRI YA KUUAWA KWA ZITTO KABWE



Katika gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘ SIRI YA KUUAWA ZITTO YAFICHUKA’ na vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ Dk. Slaa atajwa kumtuma Ben Saanane kummaliza’. 

Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:

Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.

Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.

Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.

Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.


Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar-es-Salaam
Jumatano, Machi 27, 2013

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...