PRESHA ya pambano la watani wa jadi imezidi kupanda, baada
ya Yanga kujipa mazoezi ya nguvu kusaka pumzi na stamina kabla ya kuwavaa
mahasimu wao, Simba, Mei 18 mwaka huu, huku viongozi na timu nzima wakidai
kubakiza mechi hiyo kutimiza furaha yao.
Yanga, ambayo tayari imeshatangaza ubingwa wa Ligi Kuu
Tanzania Bara msimu huu, imeona wazi kwamba hakuna sababu ya kubweteka na
kusherehekea jambo hilo hadi hapo watakapomalizana na Simba katika mechi hiyo
ya kusaka heshima kubwa.
Yanga imebainisha wazi kwamba furaha yao ya ubingwa wa ligi
msimu huu haitakamilika kama watashindwa kuifunga Simba, hivyo jambo hilo
limeifanya timu hiyo kuingia gym kupiga mazoezi ya nguvu kuhakikisha
wanatunisha misuli, kutafuta stamina na pumzi ya kuhakikisha inawatuliza
mahasimu wao kwa dakika zote tisini katika mechi hiyo itakayofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wababe hao wa mitaa ya Jangwani wamenyakua ubingwa huo
kiulaini, baada ya Azam FC kuambulia sare ya bao 1-1 juzi katika mechi yake
dhidi ya Coastal Union, matokeo ambayo yamefanya kusiwepo na timu yoyote
inayoweza kufikia pointi za Yanga (56), huku timu hiyo inayonolewa na Mholanzi,
Ernie Brandts, ikibakiza mechi mbili.
Lakini, sasa mabingwa hao wapya, Yanga wanadai furaha yao
haijakamilika kwa sasa kwa sababu bado hawajawafunga Simba na hilo ndilo
linalowafanya nyota wa kikosi hicho pamoja na benchi zima la ufundi kufanya
mazoezi ya nguvu ili kuhakikisha wanakuwa fiti katika idara zote.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, alisema
wamepokea kwa mikono miwili ubingwa huo wa msimu huu, lakini bado wana kazi
moja ya kuhakikisha mashabiki wa timu hiyo wanaendelea kupata furaha kwa
kuwafunga watani wao wa jadi, Mei 18 mwaka huu.
Akisema hatua ya kupata ubingwa mapema ni ishara kwamba
walikuwa wamejiandaa vyema, huku akiwapongeza wachezaji wake pamoja na benchi
zima la ufundi kwa kufanya kazi kwa kujituma na kudai kwamba moto huo
utaendelea hadi Mei 18 katika Uwanja wa Taifa.
“Tunaupokea ubingwa kwa furaha, lakini bado tuna kazi
nyingine, moja ni kupata ushindi dhidi ya Coastal Union na pili ni kuifunga
Simba katika mchezo wa mwisho, hizi ndizo changamoto kubwa zinazotukabili kwa
sasa," alisema.
“Kwa hiyo tunawaomba mashabiki na wapenzi wa Yanga kuendelea
kuiunga mkono timu hadi mwisho wa msimu kwa sababu tumedhamiria kuwapa raha.”
Katika hatua nyingine, Kocha mkuu wa kikosi hicho, Ernie
Brandts ameeleza kuwa pamoja na kupata ubingwa huo wakiwa wamebakisha mechi
mbili, lakini yeye bado hajamaliza ligi hadi atakapopata pointi sita
zilizobakia kwenye michezo hiyo mwili.
“Ligi haijaisha, suala la kupata ubingwa ni jambo moja,
lakini kumaliza kwa ushindi ni suala jingine muhimu zaidi, naamini kuwa hilo ni
jambo ambalo limebakia kwangu na benchi langu la ufundi kuhakikisha kuwa
tunapata pointi sita kutoka kwenye mechi zetu zilizobaki," alisema.
Kutokana na hilo, kocha huyo aliingiza timu yake katika
mazoezi ya gym, katika kituo cha mazoezi kilichopo jengo la Quality Centre
kujiandaa na mechi hizo mbili dhidi ya Coastal Union na Simba.
Kwa upande wa baadhi ya wachezaji waliozungumza jijini,
wameeleza furaha yao kutokana na matokeo hayo, lakini wakisema kuwa wanayo kazi
ya kulipa kisasi cha mabao 5-0 za msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Mbuyu Twite, ambaye alidai
ameupokea ubingwa huo kwa shangwe kubwa kwa sababu huu ni msimu wake wa kwanza
na jambo zuri kumaliza ligi akiwa na medali ya ubingwa. Kiungo wa timu hiyo,
Haruna Niyonzima, alisema jambo hilo linampa furaha kubwa na sasa anafikiria
mpango wa kufanya mazungumzo ya kuweza kubaki kwenye kikosi hicho.
Yanga, ambayo kwa sasa imefikisha pointi 56 kwenye ligi
baada ya kushuka dimbani mara 24, imebakiza mechi mbili dhidi ya Coastal Union
itakayofanyika Mei Mosi na Simba itakayofanyika siku 18 baadaye, kwenye Uwanja
wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment