Kama mabondia vile Niyonzina, Taita na Kiiza wakiwa wamevaa gloves boxers |
Haaruna Niyonzima akifanya mazoezi gym jana |
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema sasa
anakaribisha mazungumzo ya mkataba mpya kuona kama utakuwa na tija ya kumfanya
aendelee kubaki na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Nyota huyo wa kimataifa wa Rwanda, Niyonzima, aliiambia
Dimba kwamba kwa sasa yupo tayari kuketi mezani na viongozi wa Yanga
kuzungumzia mkataba mpya baada ya huu wa sasa kufika ukingoni mwishoni mwa
msimu.
Alisema kama dili hilo mpya litakuwa na maslahi basi hataona
sababu ya kuihama timu hiyo na kwamba ataendelea kukipiga katika timu hiyo
iliyonyakua taji lake la 24 la ligi msimu huu.
Kumekuwa na taarifa kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo ya
Yanga kwamba tayari wameshamsainisha mchezaji huyo mkataba wa miaka miwili,
lakini kwa kauli ya mwenyewe ni kwamba yupo tayari kuendelea kubaki mahali kama
tu wataweza kufikia makubaliano.
Alisema: "Kwanza nimefurahi sana kwa timu yangu kufanya
vizuri. Sasa nafikiria kuketi kitako na uongozi kuzungumzia hatima yangu kuhusu
suala la mkataba mpya."
Kiungo huyo amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kabisa katika
kikosi hicho cha Yanga msimu huu, ambapo kimeweza kufanikiwa kutwaa ubingwa wa
ligi uliokuwa ukishikiliwa na mahasimu wao, Simba.
Yanga, wanaonolewa na Mholanzi, Ernie Brandts, sasa
wamebakiza mechi mbili kumaliza msimu, ambapo Jumamosi ijayo watakipiga na
Coastal Union katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kumaliza na Simba
kwenye uwanja huo, siku 18 baadaye.
No comments:
Post a Comment