Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, June 18, 2013

Siitaki Tanzania ya Ugaidi na Mauaji, naitaka Tanganyika ya Amani na Utulivu!


Na Bryceson Mathias
SI UTANI; nimesema siitaki Tanzania ambayo viongozi na Watawala wake hawataki kuimba wimbo wa, Ili Tuendelee, tunahitaji vitu vinne; Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora.
Kiongozi lazima atokane na Watu, wasipokuwepo watu hakuna Kiongozi, ataongoza Mawe? Kiongozi asiyejali watu si Kiongozi; Hivyo siitaki Tanzania itakayoruhusu watu wake wauawe ovyo kama ndege, watekwe, wajeruhiwe na kuwindwa kama Wanyama au ndege.
RASHID KAWAWA
Siitaki Tanzania ambayo Viongozi wake hawatajali Uridhi wa Vizazi vya watu wake ikiwemo Ardhi. Mtawala atakayeacha watu wake wanyang’anywe na kudhulumiwa Ardhi, huyo hawapendi watu wake na wala hatokani nao. Watu wanaweza kukusaidia.
Sitaki hata kuiona Tanzania yenye siasa Chafu, Siasa ya Kuhasimiana, ya kulipizana Visasi, Siasa ya kumfurahisha mtu na kuwaumiza wengine, ya Kung’angania Madaraka, Siasa ya Nyangumi,  Mamba na ya Sumu ya Nyoka.
Sipendi kunusa, kuiona hata kuisema, Siasa ya kuviziana, kutekana na Kutupana Mabwepande, kutoana Meno, Kucha, kutoboana Macho, Kumwagiana Tindikali, ya Mabomu ya Machozi, Siasa ya Maji ya Kuwasha.
Kama Siasa ya namna hiyo itaendelea kujiri; ni heri kuishi chini ya Mkoloni, ni heri tusigambe kuwa tuna Uhuru, na ni Kheri tuitwe wanyama kama walivyotuita Wazungu, kwamba tu Masokwe watu, kutokana na tabia hiyo ya kutesana wenyewe!
Naichukia sana Siasa ya Makundi na Usultani, inayodharau watu wengine na kuwafanya waonekane kama Kinyaa, kiasi cha kuwaita huzungumzi na Mbwa, ila Mwenye Mbwa! Maana kama kilichoumbwa na Mungu kikapuliziwa Pumzi ya Uhai ni Mbwa!.........
Sithubutu kuinusa hata kuipa Mawazo Siasa ya wasiokubali kushindwa, wanaoona wako sawa, hata wanapokosea, wanaoona pekee yao ndio wanafaa kutawala, kumbe hata uwezo wa kutawala hawana! Wanaotaka wasikilizwe wao tu! Wao wasisikilize!
Natamani Mungu angerejesha, Utawala wa Tanganyika ambao ndani mwake alikuwemo Baba wa Taifa na Mwasisi wake Mwalimu Julius Nyerere, ambapo tulionekana kama tunachelewa lakini tuliheshimiwa! Na watu waliishi miaka Mingi!
Naitaka Tanganyika hiyo iliyokuwa haina Ufisadi, tofauti na wa leo wa kupindukia. Siku hizi anaweza akauawa Mtu mchana kweupe na watu wanaona na  Polisi wakishuhudia ukiporwa kila kitu, lakini wasiseme chochote!
Naipenda Tanganyika ya Bibi Titi Mohamed, ambayo ilikuwa haina Udini, iliyovaa Utu! Uadilifu na Uzalendo wa Taifa hili. Naitaka Tanganyika ya Waziri Mkuu Rashid Mfalme Kawawa (Simba wa Yuda), ambaye hata akikosolewa alikuwa anakubali!
BIBI TITI
Naitaka Tanganyika ya waliosema, Madini ardhini hayaozi hadi wazao wao wapate Akili na vifaa vya kuvunia yakiwa nchini Tanganyika, kuliko kukodi watu wayachimbue kwa madai watu wetu hawana uelewa lakini yanatoroshwa na kuwapa faida wageni.
Siitaki Tanzania ya Viongozi wanaochaguliwa kwa Rushwa na Ufisadi, wanaochukia wandishi ambao wakiwa madarakani wanarudisha kwanza fedha walizotumia kupata Uongozi, na hatimae kuwakumbuka Watanganyika kwa kuwabagua kwa Udini, na kurithishana Uongozi Kiu-koo.
Pia Sitaki hata kusikiliza, Bunge la Tanzanaia ya Leo, ambalo wabunge wake  wanasema Ndiyooo! hata kwenye Elimu Chafu! hawaungani kusema siyo kwenye siyo na ndiyo kwenye Ndiyo kama Enzi ya Tanganyika ya Spika Adamu Sapi Mkwawa.
Siitaki Tanzania ya Viongozi wanaotuhumiwa kuwa na Vyeti Bandia, au vilivyoungwaungwa kama Nywele Bandia za kuunganisha, ilihali zenyewe ni za Kipilipili, na wanaoporomosha Matusi bungeni kama Mabomba ya Maji.

Makala hii imeandikwa na

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...