Katibu wa Wabunge wa
Tanzania Katika Bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji akifafanua jambo
wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu
miswada mbalimbali iliyojadiliwa na bunge hilo kwa kipindi cha mwaka
mmoja. Kushoto ni mbunge wa bunge hilo, Abdullah Mwinyi. (Picha zote na Habari Mseto Blog)
Mbunge
wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi akizungumza na waandishi
wa habari leo. Kulia ni Katibu wa wabunge wa Tanzania katika bunge hilo,
Shy-Rose Bhanji.
DAR ES SALAAM, Tanzania
KATIBU wa Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika
Mashariki, Shy-Rose Bhanji, amejivunia harakati chanya alizoshiriki katika
kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanza kushiriki vikao vya bunge hilo Juni mwaka
jana, huku akiielezea kuvutiwa na miswada miwili inayosubiri baraka za Marais
wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Shy-Rose, alisema kuwa,
yeye kama mbunge amejifunza mengi katika miezi 12
ya uwapo wake bungeni, huku akiitaja miswada hiyo kuwa ni sheria ya
Udhibiti wa
Uzito wa Magari Barabarani ‘Vehicle Load Contol Bill’ na Punguzo la
Vituo vya
Ukaguzi Mipakani ‘One Stop Border Posts Bill.’
Aliongeza kuwa, bunge hilo limeijadili kwa kina miswada
hiyo, ambayo kwa sasa inasubiri maamuzi ya Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, huku
akitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa za Kijiografia za Afrika
Mashariki ili kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Shy-Rose alisema kuwa, sheria hizo zitakuwa na tija
kubwa kwa wananchi na mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutokana
na ughali wa ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa sasa, lakini pia urasimu
ulioshamiri katika vituo vingi vya ukaguzi wa abiria na mizigo mipakani kwa
wanaotoka nchi moja kwenda nyingine.
“Uhai wa barabara zetu Afrika Mashariki unategemea
matumizi sahihi, yanayozingatia uzito wa magari kwa barabara husika. ‘Vehicle
Load Control Bill’ ina kila kanuni itakayowabana madereva kuhakikisha wanatumia
barabara kwa uzito sahihi wa mzigo garini, ili kuzifanya zidumu kwa muda
mrefu,” alisema Shy-Rose.
Aliongeza kuwa, mawasiliano ya barabara ndio mhimili wa
maendeleo katika nchi yoyote na ili kudumisha barabara kuepuka ujenzi ghali wa
mara kwa mara, sheria hiyo imependekeza uzito wa juu kabisa kwa magari
yanayotumia barabara za Afrika Mashariki uwe ni tani 55 na sio zaidi.
Alifafanua kuwa, muswada huo umezingatia mambo mengi, hasa
kutokana na ukweli kuwa kabla ya hapo kila nchi ilikuwa na sheria yake ya uzito
wa juu zaidi barabarani, huku nchi nyingine za Afrika Mashariki zikiwa hazina
sheria hiyo na kuruhusu magari kubeba uzito wowote na kupita barabara yoyote.
Kuhusu muswada wa ‘One Stop Border Posts Bill,’
Shy-Rose alisema kuwa, ni wazi kwamba jamii ya Wana-Afrika Mashariki,
imechoshwa na urasimu mkubwa unaowakumba wanapohitaji kusafiri kutoka nchi moja
kwenda nyingine, unaosababishwa na uwingi wa vituo vya ukaguzi wa abiria na
mizigo yao, hivyo muswada huyo ni tiba ya kero hiyo.
“Sheria hii ikipitishwa na kuridhiwa na Marais wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, itamaliza hadha za usafiri zisizo za lazima,
wanazokabiliana nazo wananchi, kiasi cha kuchelewesha safari zao na kjurudisha
nyuma harakati chanya za kujiletea maendeleo yao na nchi zao kwa ujumla,”
alisema Shy-Rose.
Kwa upande wake, Mbunge mwingine wa bunge hilo,
Abdullah Mwinyi, alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imejikita kujiletea
maendeleo kupitia nyanja tofauti, zikiwamo za Forodha, Soko Huria na Sarafu ya
pamoja, ambapo Bunge hilo limejadili mengi yaliyo bora kuhusu Forodha na sasa
wanaingia katika Soko Huria.
“Soko Huria ndio kiini halisi cha mafanikio ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Dalili za mafanikio kupitia nyanja hiyo zimeanza
kuonekana, ambapo bidhaa nyingi za Afrika Mashariki zilizokuwa zikiuzwa huko
Afrika Magharibi, kwa sasa zinaingia rasmi kwenye mzunguko wa nchi wanachama wa
Afrika Mashriki na kuchangia maendeleo ya pamoja,” alisema Mwinyi.
Aidha, Shy-Rose na Mwinyi wakatumia fursa hiyo
kuwasilisha pole ya pamoja kati yao na wabunge wengine wa Bunge la Afrika
Mashariki, kwa wahanga wa bomu jijini Arusha, ambako watu kadhaa walifariki
dunia na wengine kujeruhiwa vibaya, huku wakilaani vikali shambulizi hilo
lililoathiri watu wasio na hatia.
“Tunaviomba vyombo vya dola kuhakikisha vinatumia kila
njia kuwanasa waliohusika na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria. Tunawaomba
wana Arusha na atanzania kwa ujumla kudumisha amani, upendo, utulivu na mshikamano
miongoni mwa Watanzania,” walisisitiza wabunge hao.
Kwa mujibu wa wabunge hao, vikao vijavyo vya bunge hilo
vitafanyika kama ifuatavyo: Agosti 18 hadi 29, Oktoba 13 hadi 26 vikao vitakuwa
jijini Arusha, huku Novemba 17 hadi Desemba 6 vikao vikiwa jijini Nairobi.
Desemba 19 hadi 31, Januari 9 hadi Machi 22 na Mei 25 hadi Juni 6 mwakani vikao
vyote vitafanyika jiji Arusha.
No comments:
Post a Comment