Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, June 26, 2013

AMRI KIEMBA ACHEKELEA TUZO YA SPUTANZA


Amri Kiemba akishangilia moja ya mabao yake uwanjani
KIUNGO mshambuliaji wa timu za Simba na Taifa Stars, Amri Kiemba amewashukuru waandaji wa tuzo za Mwanasoka Bora Tanzania, Chama cha Wachezaji Soka Tanzania (SPUTANZA) kwa kumpa heshima hiyo ambayo haikutarajia baada ya kutoka kwenye kipindi kigumu ndani ya klabu yake.
Akizungumza na MICHARAZO mchana huu, Kiemba alisema heshima aliyepewa na SPUTANZA ya kuwa Mwanasoka Bora kwa mwaka 2013, imemfanya ajisikie fahari na kutambua kuwa wapo wanaokubali mchango wake katika soka la Tanzania.
"Nimefurahi kwa kutwaa tuzo hii ya Sputanza, hata kama maandalizi yake yalikuwa ya haraka haraka, lakini siku zote mwanzo mgumu na ninawapongeza na kuwashukuru, nikiamini kwamba mchango wangu unathaminika kwa wadau," alisema Kiemba.
Kiemba, alisema anaamini tuzo hiyo ni changamoto kwake kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.
"Kunyatua tuzo hii ni changamoto kwangu kwa msimu ujao, watu watapenda kuona nafanya kitu gani baada ya msimu uliopita kung'ara, lakini yote kwa yote namuachia Mungu kwani yeye ndiye mpangaji wa kila jambo," alisema Kiemba baba wa watoto wawili, Shaaban na Amri Kiemba Jr.
Kiungo huyo aliyewahi kung'ara na timu za Kagera Sugar, Yanga na Miembeni amenyakua tuzo hiyo baada ya kung'ara msimu uliopita akiifungia Simba mabao 8 na pia kuipigania Stars kwenye mbio zake za kuwania Fainali za Kombe la Dunia za mwakani, japo Tanzania imekwama.
Kabla ya kurejea kwenye kiwango kilichowavutia makocha na mashabiki wa soka, Kiemba alikaa nusu msimu wa 2011-2012 bila kucheza kupinga maamuzi ya uongozi wa Simba kumtoa kwa mkopo kumpeleka timu ya Polisi Dodoma ambayo ilikuja kuteremka daraja mwishoni mwa msimu huo.
Mbali na Kiemba tuzo hizo za SPUTANZA pia ilinyakuliwa na Salum Abubakar 'Sure Boy' wa Azam kama Mchezaji Bora Chipukizi, Hussein Sharrif 'Casillas' (Kipa Bora) na kocha Mecky Mexime wa Mtibwa aliyetangazwa kuwa Kocha Bora wa Mwaka.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...