Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, August 1, 2013

CCM YAIPONGEZA SERIKALI KURUDISHA NYUMA SUALA LA WANANCHI KULIPIA KODI LAINI ZA SIMU


NA MWANDISHI WETU

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza serikali, kwa uamuzi wake kurejesha bungeni kwa ajili ya mdajala zaidi, muswada wa sheria ulioanzisha kodi mpya ya tozo ya sh. 1,000 kwa laini ya simu.

Taarifa ya CCM iliyotolewa leo mjini Dodoma, na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye imesema uamuzi huo umedhihirisha kwamba serikali inawasikiliza na kuwajali wananchi wake.

Akiripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari leo, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa amekaririwa akisema kwamba mjadala kuhusu muswada wa sheria ya kodi hiyo ya tozo hiyo utafanyika wakati wa mkutano wa Bunge unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Baada ya kupitishwa na bunge Juni mwaka huu, na utekelezwaji wake kuanza rasmi Julai mwaka huu, CCM ilikuwa miongoni mwa wadau waliopinga vikali kuanzishwa kwa kodi ya tozo hiyo, ikieleza kwamba ni mzigo na usumbufu usio wa lazima kwa watumiaji wa simu ambao wengi matumizi yao ni ya kawaida.

Katika taarifa hiyo, CCM imesema kwa kuwa wabunge wengi ni wa chama hicho, watumie fursa hiyo kuhakikisha sheria ya tozo hiyo inaondolewa na wakati huohuo watumie uwezo wao wote kuhakikisha wanaishauri serikali vizuri kupata njia mbadala itakayotumika kuziba nafasi itakayokuwa imeachwa kwa kuondolewa tozo hiyo.

"Kimsingi hatua hii imetupa faraja na hivyo CCM inaipongeza Serikali kwa kuamua kusitisha sheria ya kodi ya tozo hiyo ya sh. 1,000 kwa laini ya simu kwa kuwa ingesababisha usumbufu na adha isiyo ya lazima kwa wananchi", imesema CCM katika sehemu ya taarifa yake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...