Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, September 12, 2013

Kombe la Chalenji kupigwa Kenya Nov.


Musonye (kushoto) mbele ya Kombe la Chalenji
MICHUANO ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati mwaka huu imepangwa kufanyika kuanzia Novemba 22 hadi Desemba 8 nchini Kenya.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Nairobi, katibu mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, alisema kuwa tayari maandalizi ya mashindano hayo ya kila mwaka yameanza.

Musonye alisema kuwa anaamini nchi wanachama zitatumia mashindano hayo kuandaa timu zao kwa ajili ya michuano ijayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayofanyika mwaka 2015.
"Tumeshaanza maandalizi ya mashindano ya Chalenji na kwa asilimia mwenyeji atakuwa ni Kenya, taarifa zaidi tutaendelea kuzitoa," alisema Musonye.

Alisema kuwa sekretarieti ya shirikisho hilo imeshaanza kuwasiliana na nchi wanachama ili kuandaa timu na kutuma majina ya waamuzi watakaokwenda kuchezesha michuano hiyo.

Rais wa KFF, Sam Nyamweya, alikaririwa akizungumza jijini Nairobi mwishoni mwa wiki akisema kwamba Kenya imejiandaa kuwa wenyeji wa michuano hiyo na wanaamini watafanya vizuri kuliko miaka iliyopita.
Nyamweya alisema kuwa michuano hiyo inatarajiwa kufanyika katika miji miwili ambayo ni Nairobi na Kisumu.

"Ila bado Kisumu hawajathibitisha kuwa wenyeji," alisema rais huyo ambaye mwaka jana alishuhudia Harambee Stars ikilala dhidi ya wenyeji, Uganda (The Cranes) katika mechi ya fainali kwenye uwanja wa Mandela uliopo Namboole.

Mara ya mwisho Kenya kuandaa mashindano hayo ilikuwa ni mwaka 2009 na michuano hiyo ilifanyika Nairobi na Kakamega.

Timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) mwaka jana ikiongozwa kwa mara ya kwanza na kocha Kim Poulsen, ilimaliza katika nafasi ya nne baada ya kufungwa na 'ndugu zao' Zanzibar Heroes kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...