Jengo la Dakhalia ya Chuo cha Kilimo Kizimbani likionekana katika mandhari nzuri na ya kupendeza.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipanda mti kama
kumbukumbu mara baada ya kuizinduai dakhalia ya Chuo cha Kilimo
Kizimbani Wilaya ya Magharibi.
Makamu
wa Pili wa Raiswa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua Dahalia ya
chuo cha Kilimo kizimbani ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya
kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mkurugenzi wa Chuo cha Kilimo Kizimbani Nd. Mohd Khamis Rashid akimpatia Balozi Seif zawadi ya ndizi bora aina ya Mkono Mmoja iliyolimwa kitaalamu chuoni hapo.
***********************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vijana pamoja na wanafunzi wa Zanzibar wana fursa nzuri ya kupata elimu ya juu hapa hapa nchini kutokana na kuongezeka kwa vyuo vikuu ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
Alisema
utafiti wa Kitaalamu umebainisha kwamba mwanafunzi anayepata digirii ya
kwanza mfano Nchini Uingereza analazimika kulipiwa zaidi ya shilingi
milionio 57,000,000/- fedha ambazo zinaweza kugharamia wanafunzi kadhaa
hapa nchini wakati kiwango na ubora wa elimu kinafanana.
Balozi
Seif alieleza hayo wakati akiizindua Dakhalia mpya ya chuo cha Kilimo
Kizimbani ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“ Tumefikia wakati Zanzibar hakuna sababu kwa elimu ya diploma na digirii ya kwanza kufuatwa
tena nchi za nje hasa tabia iliyojengeka kwa vijana kwenda Ulaya kwani
tayari tumeshakuwa na vyuo vikuu vinavyotosheleza mahitaji”. Alifafanua
Balozi Seif.
Aliutaka
uongozi wa Chuo cha Kilimo Kizimbani kuongeza juhudi za kutoa Taaluma
ili Taifa likidhi mahitaji ya Wataalamu wa Kilimo ambao hivi msasa wapo
141 wakati mahitaji ni Wataalamu 287 kukiwa na upungufu wa Wataalamu
146.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba ujenzi wa dakhalia uliofanywa na chuo cha
kilimo ni mabadiliko makubwa yatakayoiwezesha Zanzibar kuwa na wataalamu
wake na kuacha mfumo wa kutegemea watalaamu wa kigeni ambao
wanaibebesha mzigo Serikali.
“
Nafurahi kuona chuo cha Kilimo Kizimbani kimezaa dakhalia ikiwa ni
ishara ya mabadiliko na mapinduzi katika sekta ya kilimo ambayo ni
tegemezi kwa Uchumi wa Taifa”. Alifafanua Balozi Seif ambae pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar.
“ Mapinduzi ya Kilimo ni
vyema yakaenda sambamba na mabadiliko ya chuo cha Kizimbani”.
Aliendelea kusisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Amewaomba
wanafunzi wa chuo hicho kujizatiti katika mafunzo yao kwa vile Serikali
kupitia Wizara ya Kilimo imeshawaandalia mazingira bora ya kujipatia
Elimu wanafunzi hao.
Alikumbusha kwamba taratibu za chuo lazima zifuatwe na wanafunzi hao katika dhana ya kudumisha nidhamu ya hali ya juu itakayokijengea sifa nzuri chuo hicho kitaifa na Kimataifa.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd. Afan Othman Maalim
alisema katika kukijengea uwezo zaidi wa kitaaluma chuo cha Kilimo Kizimbani
Wizara ya Kilimo tayari inawaandaa Walimu kumi kupata mafunzo ya ajuu
kwa ajili ya kukiwezesha chuo hicho kutoa elimu ya Digirii ya kwanza.
Nd.
Afan alisema hatua hiyo imelenga kuondosha tatizo la uhaba wa mabwana
na mabibi shamba uliopo ambao unachangia kudumaza juhudi za wakulima
katika uzalishaji wa Kilimo.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo alifahamisha kwamba mpango huo utakwenda
sambamba na juhudi za serikali kupitia wizara hiyo na kwa msaada wa Serikali ya Norway kwa kujenga dakhalia nyengine kubwa na ya kisasa muda ufupi ujao.
Akitoa
Taarifa ya Ujenzi wa dakhalia hiyo pamoja na mikakati ya baadaye ya
Chuo Mkurugenzi wa chuo cha Kilimo Kizimbani Nd. Mohd Khamis Rashid
alisema ujenzi wa dakhalia hiyo yenye vyumba saba na kuhudumia wanafunzi
42 umekuja kutokana na changamoto iliyojitokeza ya ongezeko kubwa la
idadi ya Vijana wanaotaka kujiunga na chuo hicho.
Alisema mbali ya wanafunzi wa chuo hicho lakini pia dakhalia hiyo itatumiwa na wakulima wa mafunzo na muda mfupi kipindi ambacho wanafunzi wa chuo hicho watakuwa likizoni.
Mapema
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuangalia maonyesho
ya kazi mbali mbali zinazofanywa na wanafunzi hao likiwemo zaidi suala
la utafiti wa ardhi, mazao ya kilimo na mifugo.
Walimu
wa chuo cha Kilimo Kizimbani wakiongozwa na mwalimu wa mazao katika
chuo hicho Bwana Foum Ali Garu alimueleza Balozi Seif juhudi
zinazochukuliwa na chuo hicho katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu
wanafunzi hao katika kufanya utafiti kwa vitendo.
Dakhalia hiyo ya chuo cha Kilimo Kizimbani imegharimu jumla ya shilingi Milioni 399,000,000/- na kugharamiwa na Mfuko wa Kimataifa wa kuendeleza Kilimo { IFAD }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/1/2013.
No comments:
Post a Comment