Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi
Muuguzi Mkunga wa Wodi ya Watoto waliopata ajali Bibi Leluu Omar Said
msaada wa vitanda 14, magodoro na mashuka yake kwa ajili ya wodi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwakagua watoto waliolazwa kupatiwa huduma katika wodi ya ajali Mnazi Mmoja kabla ya kukabidhi msaada kwa ajili ya wodi hiyo
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkagua mmoja wa wagonjwa wa
wodi ya Mifupa aliyelazwa kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa
vilivyotolewa na wasamaria wema.
Wafadhili na washirika wa Maendeleo wameendelea
kukumbushwa kuchangia huduma za afya kwa nia ya kuwaondoshea mzigo
wananachi pamoja na Serikali katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Kumbusho
hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi wakati akikabidhi Msaada wa Vitanda 28 pamoja na Magodoro, Mito na mashuka yake kwa ajili ya Wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Msaada
huo wa Vitanda unaokadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania Milioni
12,000,000/- unazihusu wodi ya Watoto wanaopata ajali, Wodi ya Mifupa ya
wagonjwa wa Kiume pamoja na chumba wanacholazwa wagonjwa wanaotumikia
chuo cha mafunzo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Akikabidhi
msaada huo uliotolewa na Wasamaria wema Balozi Seif alisema bado
Hospitali pamoja na Vituo vya afya hapa Nchini vinahitaji kupatiwa
misaada ili viweze kutoka huduma katika kiwango kinachokubalika.
Alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake itaendelea
kujitahidi zaidi katika kutafuta wafadhili sambamba na kuongeza nguvu
za upatikanaji wa vifaa vya huduma lengo likiwa ni kuimarisha huduma za
afya mijini na Vijijini.
Msaada huo unafuatia ziara yake Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyoifanya katika sekta ya afya mwaka
uliopita na kushuhudia changamoto kadhaa zinazovikabili vituo vingi vya
afya pamoja na Hospitali ukiwemo uhaba na uchakavu wa vitanda na
magodoro ya wagonjwa.
Wakipokea
msaada huo kwa nyakati tofauti Muuguzi Mkunga katika wodi ya Watoto
Bibi Leluu Omar Said na Muuguzi dhamana katika Wodi ya Mifupa ya
Wagonjwa wa Kiume Bibi Afsa Abdulla wamewashukuru wafadhili hao kupitia
Balozi Seif kwa msaada wao utakaosaidia kupunguza matatizo
yanayozikabili hospitali hiyo.
Wauguzi wakuu hao wa wodi hizo wameahidi kwa pamoja kuvitunza Vifaa hivyo ili vidumu kwa muda mrefu kwa vile changamoto hilo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.
Hata
hivyo wauguzi hao wameiomba serikali kufanya utaratibu wa hifadhi zaidi
ya magodoro hayo ili yadumu zaidi suala ambalo Balozi Seif aliuagiza
Uongozi wa Wizara ya Afya kulifanyia kazi mara moja.
Mapema Balozi Seif alipata fursa ya kuwakagua waonjwa waliolazwa katika wodi zilizofanikiwa kupata msaada wa Vitanda, magodoro pamoja na Mashuka.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kutoa
msaada kama huo hivi karibuni katika Hospitali za Micheweni na Vitongoji
Kisiwani Pemba.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/1/2013.
No comments:
Post a Comment