Na Elizabeth John
SHIRIKISHO la Mchezo wa Bao Tanzania (SHIMBATA), limewaomba
wadau kujitokeza kudhamini mchezo huo ili kufanikisha kuendesha shindano la
kumuenzi Baba wa Taifa Mwl. JK Nyerere, ambalo limepangwa kuanza Octoba 10 hadi
13 Mkoani Shinyanga.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa SHIMBATA,
Monday Likwepa alisema hadi sasa hawana ufadhili wowote ambao umejitokeza
kudhamini ili kufanikisha mashindano hayo, ambayo yatashirikisha mikoa 11 ya
Tanzania bara na mmoja kutoka visiwani Zanzibar.
“Gharama ambazo zitatuweza kufanikisha mashindano hayo ni
milioni 59, ambapo zitakuwa ni gharama za wachezaji wa mikoa yote kwa huduma za
maradhi na chakula ambapo kila Mkoa utaleta wachezaji sita,” alisema Likwepa.
Mbali na mashindano hayo, SHIMBATA wameandaa mikakati
endelevu ikiwemo uundwaji wa vyama vya mikoa, uendeshaji wa mashindano
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushiriki mashindano ya kimataifa.
“Mchezo wa Bao ni Mchezo wa Kitanzania tena wa Kizalendo na
ndio mchezo pekee uliosaidia harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kwa upande wa
Bara na Visiwa vya Zanzibar kama eneo muhimu la kukutania kupanga mikakati ya
kuung’oa ukoloni. Hivyo unatakiwa upewe heshima ya kutosha,” alisema Likwepa.
Aliongeza kuwa SHIMBATA wameanza majadiliano ya kuuingiza
katika orodha ya michezo inayotumia akili zaidi Duniani kutoka Chama cha
Kimataifa (IMGA) na kwamba wana uhakika wa kuchukua medali za mchezo huo ikiwa
mwaka 2016 utafanikiwa kuingizwa katika mashindano ya Olimpiki.
No comments:
Post a Comment