Mshambuliaji wa Simba, Mrisho Ngasa akimiliki mpira mbele ya beki wa Ruvu Shooting
Golikipa wa
timu ya Ruvu Shooting, Benjamin Haule akijaribu kuokoa mpira uliopigwa
na beki wa Simba, Shomari Kapombe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka
Tanzania Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam. Simba ilishinda 2-1. (Picha na Habari Mseto Blog)
Mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu akichuana na beki wa Ruvu Shooting
Shabiki wa Simba
Wachezaji wa Simba wakishangilia bao la kwanza la lililofungwa na Felix Sunzu
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Simba, wameendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100, baada ya kuibuika na
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, pambano lililochezwa leo kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakionekana kupania kuendeleza ubabe kwa timu za Ligi Kuu,
Simba ilianza mechi hiyo kwa kusakata soka safi na kushambulia mfululizo, huku
safu yake ya mbele ikionekana kuipa wakati mgumu idara ya ulinzi ya Ruvu.
Mfululizo wa mashambulizi ya Simba uliofanywa kwa dakika
tofauti na wakali wakali wake Daniel Akuffor, Felix Sunzu, Mrisho Ngasa,
uliwalazimu walinzi wa Ruvu Shooting kuelemewa na kufanya madhambi ya mara kwa
mara, ambapo beki George Michael alilambwa kadi ya njano dakika ya 23.
Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha, alilazimika kumuonya
Michael kwa kadi hiyo, kutokana na rafu aliyomchezea Akuffor, aliyeingia mara
kwa mara langoni kwao, ingawa hakuwa makini kutumia mipira ya viungo Amri
Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 30, likiwekwa
nyavuni na nyota wa kimataifa wa Zambia, Sunzu kwa kichwa maridadi akimalizia
krosi iliyopigwa baada ya kazi nzuri ya kuwachambua mabeki iliyofanya na Said
Nassor ‘Cholo’ aliyepanda kusaidia mashambulizi.
Dakika 38, Kiemba akawachachafya wachezaji wa Ruvu, kabla ya
krosi yake kukosa mmaliziaji na kuishia mikononi mwa Benjamin Haule.
Simba iliendelea kushambulia ambapo katika dakika ya 44, beki Mau
Bofu wa Ruvu alimwangusha Sunzu ndani ya 18 na mwamuzi Swai kuamuru ipigwe penati. Akuffor
akabeba jukumu la kupiga tuta hilo, ambalo mlinda mlango Haule alipangua na
kuwa kona tasa.
Hadi mapumziko, Simba ilitoka ikiongoza kwa bao hilo, huku
mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wakishuhudia maamuzi tata ya mwamuzi Swai,
aliyeonekana dhahiri kutowajali vibendera wake Samwel Mpenzu na Godfrey Kihwili
wote wa Arusha pindi wanapoashiria madhambi.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kushambulia lango la
Wekundu na kama si umakini mdogo miongoni mwa washambuliaji wake Paul Ndauka,
Hussein Said na Hassan Dilunga aliyekuwa akipenya kirahisi safu ya ulinzi,
wangeweza kupata mabao.
Sunzu akafanya shambuliazi kali dakika ya 55 lililotokana na
jitihada binafsi akiwalima chenga mabeki, kabla ya Ruvu nao kurudi langoni mwa
Simba na Dilunga (Hassani) nusura aipatie bao timu yake, kabla ya mawasiliano
madogo na Abdulrahman Mussa kumgharimu.
Ruvu ikapata bao la kusawazisha mnamo dakika ya 78,
lililowekwa nyavuni na mtokea benchi Seif Rashid, akitumia makosa ya beki Juma
Nyoso wa Simba, aliyeshindwa kuondoa hatari langoni akiwa peke yake na
kuukanyaga mpira huo na kuteleza, ambapo Seif aliunasa na kumchambua Juma
Kaseja.
Wakati wengi wakimiani matokeo ya pambano hilo yangebaki
kuwa ni sare ya bao 1-1, mtokea benchi wa Simba, Christopher Edward aliyeingia
kuchukua nafasi ya Akuffor, akaipatia timu yake bao la pili dakika ya 87 kwa
shuti na kuamsha mamia ya mashabiki wake jukwaani.
Katika mechi hiyo, Simba ilionekana kutawala mchezo, lakini
umakini mdogo mbele ya lango alionao mshambuliaji aliyesifiwa sana kabla ya
kunza ligi hii, Akuffor ukaendelea kuzua maswali, kabla ya baadhi yao kulaumu
kwa kumchelewesha Christopher, yoso aliyewapa ushindi huo.
Vikosi, Simba; Juma Kaseja, Nassor Cholo, Amir Maftah,
Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Amri Kiemba/Koman Keita, Mwinyi Kazimoto,
Ramadhani Chombo/Haruna Moshi, Felix Sunzu, Daniel Akuffor/Christopher Edward
na Mrisho Ngasa.
Ruvu Shooting; Benjamini Haule, Michael Pius, Mau Bofu,
George Michael, Said Suzan, Gideon David, Abdulrahman Mussa, Hassan Dilunga,
Paul Ndauka/Seif Rashidi, Hussein Said na Said Dilunga.
Kutoka Tanga, mwandishi Ahmed Khatib anaripoti kuwa, Mgambo
JKT imeshindwa kutumia vema dimba la nyumbani la Mkwakwani jijini humo, baada
ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar, shukrani kwa bao la
Kamana Salum, dakika ya 63.
No comments:
Post a Comment