Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, September 28, 2012

BONDIA RAJABU MAOJA AELEKEA NAMIBIA


. Ataiwakilisha Tanzania kwenye programu ya “IBF Utalii wa Michezo” (IBF Sports Tourism)

. Anakutana na bingwa wa Namibia kwenye mpambano wa IBF Africa.


Mtanzania Rajabu mtoto wa Jumanne Maoja mkazi wa jiji la Tanga anaondoka na Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini (South African Airways) kuelekea jijini Windhoek, Namibia ambako ana kibarua kikali kuiwakilisha Tanzania kwenye IBF Utalii wa Michezo (IBF Sports Tourism).

Maoja atakutana na bingwa wa nchi ya Namibia, Goettlieb Ndokosho kwenye mpambano uliopewa jina la “Vita Vya Jangwa la Kalahari” (The Battle for the Kalahari Desert) na waandaaji wa mpambano huo wa raundi 12 kumpata bingwa wa IBF Afrika katika uzito wa unyoya. Kinda Boxing Promotions inayoongozwa na bwana Simon Nangolo ambaye ni mkaguzi mwandamizi wa ndani wa mahesabu (Senior Internal Auditor) nchini Namibia ndio waandaaji wa mpambano huo wakukata na shoka.

Mshindi wa mpambano huo atakutana na bingwa wa IBF Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi, Mtanzania Ramadhani Shauri ambaye hivi karibuni alimkung’uta bondia Sande Kizito wa Uganda katika mpambano ulioishia raundi ya 8 baada ya Kizito kushindwa kuendelea.

Huu unakuwa mpambano wa tatu kwa Watanzania mwaka huu kuwania ubingwa wa IBF katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati ya Ghuba ya Uajemi ambako tayari mikanda miwili ya IBF iko Tanzania.

Mpambano wa Mtanzania Rajabu Jumanne Maoja na Goettlieb Ndokosho wa Namibia utafanyika katika jiji la Windhoek, mji mkuu wa nchi ya Namibia tarehe 29 Septemba siku ya Jumamosi.

Mtanzania Rajabu Jumanne Maoja atafuatana na Kocha wake Ibrahim Raphael Jorum ambaye naye anatoka katika jiji la Tanga.

Msimamizi mkuu wa mpambano huo ni Mtanzania Onesmo Alfred McBride Ngowi ambaye atalisimamia pambano hilo lililo na upinzania mkubwa!

Mungu mbariki Rajabu Jumanne Maoja, Mungu ibariki nchi nzuri ya Tanzania.

Imetolewa na:
Utawala
KAMISHENI YA NGUMI ZA KULIPWA NCHINI (TPBC)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...