Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo akizungumza na waandishi wa habari
Na Elizabeth John
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari
Lager, leo imetangaza zawadi za washindi wa mashindano ya Safari Pool Taifa
yanayotarajiwa kufanyika Septemba 26 hadi 29, mwaka huu jijini Mwanza kwa
kushirikisha mabingwa wa klabu kutoka mikoa 16 ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo,
Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo alisema zawadi kwa bingwa wa
fainali za Safari Pool Taifa 2012 ni pesa taslimu shilingi milioni tano, Kombe
na Medali za dhahabu kwa washindi wa upande wa timu.
Shelukindo alisema kuwa, zawadi za washindi wa pili itakuwa
ni shilingi 2,500,000, huku washindi wa tatu wakiondoka na kitita cha shilingi
1,250,000, ambapo washindi wa nne watajinyakulia shilingi 750,000.
Alisema kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja, mshindi kwa
wanaume atajinyakulia kiasi cha shilingi 500,000, huku bingwa wa wanawake akinyakua
shilingi 350,000 na mshindi wa pili wanaume atapata shilingi 250,000.
Mshindi wa pili kwa wanawake, ataondoka na shilingi 200,000
na mshindi wa tatu kwa wanaume atapata shilingi 200,000, huku mshindi wa nafasi
hiyo kwa wanawake akiondoka na kitita cha shilingi 150,000.
Katibu wa Chama cha Pool Taifa (TAPA), Amos Kafwinga,
alizitaja klabu zilizofuzu kushiriki fainali za Taifa jijini Mwanza kuwa ni
Balele ya Tanga, Mbosho ya Kilimanjaro,
2 Eyes ya Arusha, Janja Wild ya Manyara, Sabasaba ya Lindi na Texas ya Tabora.
Nyingine ni New Stand ya Shinyanga, Anatory ya Morogoro,
Atlantic ya Dodoma, Nginja ya Iringa, Blue House
ya Mbeya, Sun City ya Temeke, Kayumba ya
Ilala, Meeda kutoka Kinondoni, huku wenyeji wa mashindano hayo Mwanza
wakitarajiwa kuwakilishwa na klabu ya Paseansi.
No comments:
Post a Comment