TIMU
ya wasichana ya Tanzania imekabidhiwa zawadi ya Sh milioni 16 baada ya
kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 ya
Kimataifa ya Airtel Rising Stars iliyofanyika Septemba mwaka jana nchini
Nigeria.
Timu hiyo ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Kenya bao 1-0 lililofungwa na Donisia Daniel katika fainali hiyo. Akipokea
fedha hizo jana (Februari 10, 2014) Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Msanifu Kondo alisema.
wanaishukuru
Kampuni ya Airtel kwa kutimiza ahadi yao ya zawadi ya fedha hizo na
tayari wamezikabidhi kwa makocha na wachezaji wa timu hiyo.
Alisema
kila mchezaji amepewa Sh 850,000 wakati kocha mkuu wa timu hiyo
Rogasian Kaijage amepewa Sh milioni moja na laki mbili na kocha msaidizi
amepewa Sh milioni moja. “Tunawashukuru Airtel kwa kutoa fedha hizo za zawadi kwa timu hii na sisi tumewakabidhi wahusika,” alisema.
Kwa
upande wake Afisa Uhusiano wa Airtel Tanzania Jane Matinde alisema wao
kama wadhamini wa mashindano hayo wametimiza ahadi yao kwa kukabidhi
fedha hizo kwa mabingwa hao.
“Kwa
niaba ya Airtel Tanzania tunaipongeza timu ya wasichana ya Tanzania kwa
kutwaa ubingwa huo, lakini pia tumetekeleza ahadi yetu ya kukabidhi
zawadi, kama mnavyofahamu kampuni yetu imekuwa mstari wa mbele katika
kusaidia mambo ya kijamii lakini pia michezo ikiwemo soka kupitia
michuano ya vijana ya Airtel Rising Stars kwa kushiriki na klabu ya
Manchester United,” alisema.
Mohamed Mharizo
Ofisa Habari wa DRFA
Februari 11, 2014
No comments:
Post a Comment