Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, February 16, 2014

Mbunge Ndungulile aanika siri mpya za matumizi ya madawa ya kulevya kwa watoto wadogo


Mgeni rasmi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kigamboni Ndugu Faustine Ndungulile akifungua rasmi Baraza la kazi la UVCCM (W) Temeke mbele ya Wajumbe (hawapo pichani) lililofanyika kwenye ukumbi wa Malaika uliopo Kata ya vijibweni, Jimbo la Kigamboni. Picha na Emmanuel J. Shilatu
---------------------------------------
Na Emmanuel J. Shilatu
Mbunge wa Kigamboni Mhe. Faustine Ndungulile ameanika siri na aina mpya ya wauzaji wa madawa ya kulevya wanayoitumia katika kupanua wigo wa watumiaji wa madawa ya kulevya Duniani kupitia watoto wadogo.
Mhe. Ndungulile aliyasema hayo wakati akifungua Baraza la Vijana la Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia wilaya ya Temeke uliofanyika katika ukumbi wa Malaika ambapo alibainisha bayana kuwa wauzaji wa madawa ya kulevya wamekuja na mtindo mpya wa kuwafundisha watoto wadogo kutumia madawa ya kulevya kupitia kwenye vyakula wanavyopewa wakiwa mashuleni pamoja na kwenye pipi ambazo watoto hao wanapozilamba taratibu huanza kujifunza kutumia madawa ya kulevya na hata katika siku za usoni inawawia vigumu watoto hao kuacha matumizi ya madawa hayo.
“Wauzaji wa madawa ya kulevya ni watu hatari sana kwani siku hizi wameanzisha mtindo wa kuwachanganyia watoto wadogo kwenye vyakula pamoja na kuyapaka madawa hayo ya kulevya kwenye pipi ambazo watoto hao wanapozilamba huanza kujifunza matumizi ya madawa ya kulevya tangu wakiwa watoto na ni ngumu kuchomoka katika mtego wa matumizi ya madawa hayo katika maisha yao”, alisema Mhe. Ndugulile.
Kama haitoshi Mhe. Ndungulile alianika bayana matatizo makubwa yanayowasibu vijana kwa sasa kuwa ni madawa ya kulevya pamoja na maambukizi ya virusi vya ukimwi ambapo alibainisha waziwazi kuwa nguvu kazi ya taifa la leo imekuwa rehani kupitia mitego hiyo.
Mbunge huyo wa Kigamboni ambaye kitaaluma ni Daktari aliweka waziwazi kuwa licha ya takwimu za kushuka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi kushuka kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 5.1 bado tatizo ni kubwa kupita maelezo kwa vijana nchini.
“Kati ya vijana wa kike watatu wanaotumia madawa ya kulevya, wawili kati yao ambao ni asilimia 67 wameathirika na virusi vya ukimwi. Halikadhalika kwa upande wa vijana wa kiume wawili wanaotumia madawa ya kulevya, mmojawao ambaye ni asilimia 50 ana maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hali ni mbaya sana kwa vijana.”Alisema Mhe. Ndungulile.
Mbunge huyo wa Kigamboni aliwaasa wajumbe hao wa Baraza la UVCCM (W) Temeke na vijana wote nchini kuwa mbali na matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake wajibiidishe zaidi katika kufanya mambo yenye faida kwao kupitia shughuli za kiuchumi kwa kuchangamkia fursa zilizopo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...