Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, November 16, 2012

IBRAHIMOVIC: WAINGEREZA SASA LAZIMA WANIHESHIMUSTOCKHOLM, Sweden
"Ndivyo walivyo Waingereza. Ukifunga dhidi yao wewe ni mzuri, usipowafunga wao, wewe kwao sio mzuri. Ilikuwa hivyo kwa Messi kabla ya mwaka 2009 akiwa Barcelona ... kisha akafunga dhidi ya Manchester United na ghafla akawa Mchezaji Bora wa Dunia"
MSHAMBULIAJI Zlatan Ibrahimovic anaamini amewazima midomo milele wakosoaji na wasiomkubali miongoni mwa Waingereza, baada ya kufunga mabao manne likiwamo la ‘tik-tak’ mwishoni mwa mchezo kuipa Sweden ushindi wa 4-2 dhidi ya England.
Ibrahimovic alikuwa kwenye kiwango cha juu katika pambano hilo kiasi cha kumwagiwa sifa hata na nahodha wa ‘Three Lions,’ Steven Gerrard, ambapo sasa mkali huyo wa Paris Saint-Germain ya Ufaransa anasema kipaji chake hakikuwa kikikubalika England, hadi sasa.
"Kwamba hali ya mambo iko hivyo kwa Uingereza," alisema Ibrahimovic na kuongeza: "Kama ukifunga dhidi yao wewe ni mchezaji mzuri, kama hauwezi kuwafunga wao, daima wewe kwao sio mchezaji mzuri.
"Nakumbuka Lionel Messi kabla ya mwaka ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2009 akiwa na Barcelona ... kisha akafunga dhidi ya Manchester United na ghafla akawa Mchezaji Bora wa Dunia.
"Labda sasa wao wanaweza kusema kitu kama hicho kuhusu mimi," alijinasibu Ibrahimovic aliyeihama AC Milan kiangazi kilichopita na kutua PSG ya Ufaransa.
Nyota huyo mwenye miaka 31, alifunga bao bora zaidi likiwa la nne, wakati alipotegea uokozi wa kichwa nje ya boksi wa mlinda mlango wa England, Joe Hart kisha kupiga ‘tik-tak’ kali kufunga bao hilo akiwa umbali wa mita 30 katika lango tupu.
Ni bao lililomsukuma Ibra kuvua fulana yake kushangilia, akifikisha idadi ya mabao 39 katika mechi zake 85 akiwa na timu ya taifa ya Sweden.
"Hart alifanmya kosa kubwa kuchomoka langoni nami nikatumia nafasi hiyo kujaribu kupata bao. Nikiwa dimbani nikaona ‘tik-tak’ yangu ikienda kama nilivyotaka.
"Ghafla nikamuona beki wa England akijaribu kuzuia bao hilo, nikajikuta nataka kupiga kelele kusema 'Hapana' lakini mpira huo ukatii maombi yangu na kutinga kimiani.
"Hata kama ilikuwa ni mechi ya kirafiki lakini niliamua kuonesha namna gani nilivyopata furaha ya ajabu kufunga bao hilo. Ni ngumu kuelezea nilivyojisikia. Nilifurahishwa mno na kilichotokea," alibainisha Ibrahimovic.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...