Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, November 15, 2012

Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaendelea na Awamu ya Nne ya kukusanya maoni
                                                                   JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
                                                                        TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
                                                                                                     __________
 
Jumatano, Novemba 14, 2012

Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuendelea na awamu ya nne na ya mwisho ya mikutano yake na wananchi wa mikoa sita kuanzia siku ya Jumatatu, Novemba 19, 2012 hadi Jumatatu, Desema 19, 2012 kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini Magharibi na kila siku kutafanyika mikutano miwili, wa kwanza utaanza saa 3:00 asubuhi – saa 6:00 mchana na kufuatia na mwingine utakaoanza saa 8:00 alasiri – saa 11:00 jioni.

Taratibu zote za kuanza kazi ya kukusanya maoni katika mikoa iliyotajwa zimekamilika zikiwemo kuandaa ratiba na kuisambaza katika ofisi za mikoa, wilaya na Halmashauri za Manispaa na Wilaya husika. Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi saba. Kila mkoa utakuwa na kundi moja isipokuwa Dar es Salaam ambao utakuwa na makundi mawili.

Katika mkoa wa Dar es Salaam Tume imejigawa katika makundi mawili na siku hiyo ya Jumatatu itaanza na Wilaya za Temeke na Ilala. Katika wilaya ya Temeke, Tume itaanza na eneo la Keko wakati katika wilaya ya Ilala itaanza na eneo la Jangwani kwa mikutano itakayoanza saa 3:00 asubuhi. Kwa mikutano ya alasiri, wilayani Temeke mkutano huo utafanyika Chang’ombe na ule wa Ilala utafanyika Tabata.

Kwa upande wa mkoa wa Arusha, Tume itaanza na Wilaya ya Karatu eneo la Mbulumbulu wakati mkoani Mara Tume itaanza katika Wilaya ya Tarime eneo la Bumera. Kwa mkoa wa Simiyu, Tume itaanza na Wilaya ya Busega eneo la Lamadi na mkoani Geita, Tume itaanza na Wilaya ya Chato eneo la Kachwamba. Kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Tume itaanza katika Wilaya ya Magharibi.

Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa kuzungumza na pale wanapokosa nafasi ya kuzungumza, watumie fursa ya kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kwa kutumia fomu maalum zitakazokuwa zinatolewa na Tume katika mikutano hiyo.

Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia anuani za zifuatazo:

Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P. 1681, DAR ES SALAAM, Simu: +255 22 2133425, Nukushi: +255 22 2133442; Au

Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769

Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na utulivu.

Mwisho.
Imetolewa na:
Assaa Rashid,   
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM
+255 (0) 0757 500 800 / 0717 084 252

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...