Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, November 8, 2013

DKT.MVUNGI APELEKWA AFRIKA YA KUSINI KWA MATIBABU ZAIDI


 Mke wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi,(kulia) pamoja na marafiki wakiomba dua leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere dakika chache kabla na Dkt. Mvungi hajasafishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia. Dkt. Mvungi alivamiwa na kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.
Dkt. Mugisha Clement Mazoko wa Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) (kushoto), Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid (mwenye tai) na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Bw. James Mbatia (wa pili kulia) pamoja na ndugu na jamaa wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi wakiangalia wakati Mjumbe huyo akipandishwa ndani ya ndege kusafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Dkt. Mvungi alivamiwa na kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.
*************************************************
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) amesafirishwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) saa 5:45 asubuhi kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Akiwa nchini Afrika Kusini, Dkt. Mvungi atapata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg.

Itakumbukwa kuwa Dkt. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013. Tukio hilo la uvamizi linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini. 

Tangu siku alipojeruhiwa, Dkt. Mvungi alikuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI). Hata hivyo, Madaktari waliokuwa wakimtibu MOI, walishauri afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi. 

Dkt. Mvungi ameondoka na ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink na ameambatana na Dkt. Mugisha Clement Mazoko kutoka MOI; Muuguzi Bi. Juliana Moshi; na mtoto wa kaka yake Bw. Deogratias Mwarabu. Serikali inagharamia gharama zote za matibabu ya Dkt. Mvungi.

Tume inawaomba wananchi wote waendelee kumuombea kwa Mungu Dkt. Mvungi ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida na hatimaye kuendelea majukumu yake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...