Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, November 8, 2013

RAIS JAKAYA KIKWETE ALIHUTUBIA TAIFA KUPITIA BUNGE MJINI DODOMA LEO, SOMA HOTUBA YAKE HAPA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akilihutubia Bunge mjini Dodoma leo.
Rais Jakaya Kikwete akiendelea kulihutubia Bunge..........
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Mohammed Gharib Bilal,akiwasili katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo kusikiliza Hotuba ya Rais.
 ************************************************
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;

          Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
          Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali.  Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache zilizopita.   Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”.  Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.

Mheshimiwa Spika;
          Hayo si makusudio yangu.  Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo.  Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo.  Nimeona ni vyema nifanye hivyo.

Mheshimiwa Spika;
  Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake.  Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka.  Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.  Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata.  Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya.  Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.

Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
          Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo.  Kwa kweli hali inatisha.  Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...