Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Ali Mohamed
Shein,akitoa Risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kwa wananchi na
kuwataka kufanya Ibada kwa Bidii,hata hivyo Mhe, Rais
aliwakumbusha wananchi kufanya mambo muhimu yaliyowajibu kufanywa katika
mwezi huu ili kufanikiwa hapa Duniani na kesho Akhera twendako. Picha na Ramadhan Othman,Ikulu
********************************************
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa misingi ya kutodhulumiana katika bei, viwango na vipimo hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akisoma risala ya Ramadhani kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa mwaka huu wa 1433 Hijriya sawa na mwaka 2012 Miladia.
Katika
maelezo yake Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni
wa neema kibiashara lakini ni vyema kufanya neema hiyo iwe kwa wauzaji
na kwa wanunuzi.
Alieleza
kuwa Muuzaji anauza bidhaa zake nyingi zaidi kwa hivyo anapaswa
kuhakikisha zina ubora na anachuma faida kwa kiasi ya anachouza.
Aidha,
alisema kuwa mnunuzi naye anahitaji kupewa bei iliyo nafuu hasa kwa
bidhaa ambayo Serikali imeipunguza kodi, kwani Serikali kama kawaida
itapunguza ushuru kwa biadhaa muhimu za chakula ili kuwawezesha wananchi
kupata unafuu wa bei.
“Ni
jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wafanyabiashara wenye
tamaa wanasafirisha bidhaa kama vile unga, sukari na mchele walizotozwa
kodi ya chini na kuzisafirisha kwa njia ya magendo nje ya Zanzibar
ili wapate faida kubwa’,alisema Alhaj Dk. Shein.
Kutokana
na mambo hayo Alhaj Dk. Shein alisema kuwa husababisha upungufu wa
baadhi ya vyakula na kuwasababishia shida wananchi wakati huu wa mwezi
wa Ramadhani.
Pamoja
na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani kwa wakulima nchini kwa
kujiandaa kuwaopa huduma nzuri wananchi hasa katika upatikanaji
wa chakula kwa ajili ya futari huku akieleza kuwa serikali
imeweka mazingira mazuri ya biashara hasa katika Mwezi huo wa Ramadhani.
Alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nayo itajitahidi kufanya kila
linalowezekana ili kuwasaidia wananchi katika kukabiliana na tatizo la
upatikanaji wa maji katika maeneo mbali mbali nchini.
Alhaj
Dk. Shein alisema kuwa Serikali imo katika juhudi za
kuwaandalia wananchi wake maisha bora, kwa kupitia mageuzi ya katiba na
pia kwa kuhesabiwa watu, mambo ambayo yamo katika sheria.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu rehema,na kujaalia subira
huku akielezea juu ya tukio la kuzama kwa meli ya MV SKAGIT ambapo
alieleza kuwa tayari maiti nyengine 22 tokea asubuhi ya leo hadi anatoa
risala yake tayari zimeokolewa.
Alhaj
Dk. Shein pia, alitoa wito kwa wananchi kuwa watendaji wema na hisani
baina yao na hasa kwa masikini na wasiojiweza ambapo utoaji sadaka ni
jambo la msingi na hakuna budi kulizingatia zaidi katika mwezi huo wa
Ramadhan ili wale wenye kipato cha chini nao uwe ni mwezi wa furaha
kwao.
Alisema
kuwa kwa kuwa Ramadhani mwaka huu imekuja katika msimu wa Watalii na
ziara za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje, inapaswa kwa umoja wao
kuonesha wema wao na mambo mema kwao na kudumisha sifa ya
ustaarabu, uvumilivu, mshikamano na kuelimishan kwa upole kwa yale wasiyoyajua ya mila za Kizanzibari.
Aidha
aliwataka wananchi wasiowajibika na saumu kama kawaida
watoe ushirikiano na wawe wastahamilivu kwa wenzano wanaofunga na
wajitahidi kutumia fursa hiyo vyema bila ya kuwakirihisha wengine.
Alhaj
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea
kuimarisha ulizni wa watu na mali zao kwa kushirikiana na vijana wa
ulinzi shirikishi ili wananchi wapate utulivu na watekeleze
saumu kwa amani.
Dk.
Shein aliwataka wazazi na walezi nao kuzisimamia vyema nyendo za watoto
wao katika mwezi huo na kuwahimiza zaidi katika ibada na darsa. Pia,
Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kuutumia muda mwingi kuisoma na
kupata maarifa ya Qur-an katika Mwezi huu wa Ramadhan, mafunzo ambayo yatadumi siku zote.
Wakati
huo huo, viongozi kadhaa walifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya
kumpa pole Dk. Shein pamoja na wananchi kwa ujumla kufuatia ajali ya
kuzama kwa meli ya MV SKAGIT na kusababisha vifo pamoja
na majeruhi. Miongoni mwa viongozi hao ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Kharib Bilal pamoja na ujumbe wa
Wabunge 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na
Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Shamsi Vuai Nahodha.
Imetolewa na Rajab Mkasaba
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment