Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji (ambayo katika uamuzi huu
itarejewa kama ‘Kamati’) iliyokutana Julai 17 mwaka huu, baada ya
kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na mchezaji Kevin Yondani
katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili katika mashindano ya
Kombe la Kagame kama zilivyowasilishwa mbele yake imefikia uamuzi
ufuatao;
1. Kwa
mujibu wa mapitio ya nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa
upembuzi yakinifu, Kamati iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala
zima la mchezaji Kevin Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa
Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na Klabu ya Simba kwa suala hilo la
kiutendaji kama Sekretarieti ilivyofanya katika barua yake ya Julai 14
mwaka huu ulikuwa sahihi.
2. Kamati
ilibaini kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba
ulimalizika Mei 31 mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji
Kevin Yondani kuanzia Juni 1 mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.
3. Aidha
Kamati ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa
na maana ya kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin
Yondani na Klabu ya Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni
kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu
kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao
wakati mkataba halisi haujaisha muda wake. Hivyo mkataba huo kwa jicho
la
kisheria haupo.
4. Hata
kama kamati ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba
huo una tatizo la kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika
ziliingia makubaliano hayo. Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa,
wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka
jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana
iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey
Nyange Kaburu,
Desemba 23 mwaka huu.
5. Kisheria
utata huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari
hiyo kwa maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha
mabadiliko hayo. Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi
kutumika kumzuia mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati
akiwa huru.
Kutokana
na maelezo yote hapo juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa na
Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu
ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment