Wananchi wakivuka kwa miguu katika
Daraja la Manung’una, lililopo katika Kijiji cha Msisi, Singida ambalo
limekatika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
MVUA zinazoendelea kunyesha mkoani
Singida, zimesababisha maafa makubwa baada ya watu wawili, mmoja akiwa
raia ya China, kufariki dunia kwa kusombwa na maji, huku mamia ya abiria
wakikwama njiani baada ya daraja linalounganisha mkoa huo na mingine
kukatika. Kukatika kwa Daraja la Munung’una kwa siku mbili sasa,
kumesababisha msongamano mkubwa wa magari yanayokadiriwa kuwa zaidi ya
300.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza
kuwa waliofariki dunia kutokana na mvua hizo ni Xue Hui (36), maarufu
kwa jina la Kevin na Mariamu Samweli (18), mkazi wa Kijiji cha Maluga
ambao walifariki dunia kwa nyakati tofauti baada ya kusombwa na maji.
Vifo vyao vimeongeza idadi ya watu
waliofariki dunia kutokana na mvua mkoani Singida kufikia sita katika
siku tatu zilizopita. Mvua za juzi, zilisababisha watu wanne wa familia
moja katika Wilaya ya Mkalama kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na
nyumba ya tembe.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Ole Lenga
alisema raia huyo wa China, alifariki dunia juzi jioni katika Kijiji
cha Gumanga Wilaya ya Mkalama baada ya gari alilokuwa anasafiria
kusombwa na maji... “Mchina huo alikuwa na mtoto wake ambaye alinusurika
kifo.”
Alisema Mariamu alifariki dunia baada
ya kusombwa na maji katika Mto Kiula uliopo katika Kijiji cha Igonia.
“Miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha
Hospitali ya Mkoa wa Singida.”
Abiria wakwama Mvua hizo kubwa
zilizonyesha tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana, zilisababisha daraja
hilo la Munung’una lililopo katika Kijiji cha Msisi wilayani Singida
kuvunjika.
Kutokana na athari hiyo, kumekuwa na
msongamano mkubwa wa magari baada ya mawasiliano kati ya Singida na
mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani kukatika.
Baadhi ya wananchi walilalamikia uharibifu huo wakisema umetokana na ujenzi wa daraja hilo kuwa wa kiwango cha chini.
Dereva, George Medadi akitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam, alisema
daraja hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kujengwa chini ya kiwango.
No comments:
Post a Comment