Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu Kiongozi wa Japan, Yoshihiro
Suga, wakati alipofika ofisini kwake Jijini Tokyo Japan leo Mei 21,
2014, akiwa katika ziara ya kikazi.
****************************************************
Mwandishi Maalum, Tokyo
Serikali
ya Japan imeelezea nia yake ya kuendelea kuchangia bajeti ya Tanzania
na kufafanua kuwa, inafanya hivyo kwa kutambua kuwa Tanzania ni mshirika
mkubwa wa maendeleo na kwamba ni nchi yenye kutia matumaini katika
kupiga hatua za kimaendeleo.
Akizungumza
jana katika Ofisi yake jijini Tokyo, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa
Japan Mheshimiwa Yoshihide Suga alisema, serikali ya Japan inaifahamu
Tanzania kama mshirika wa maana katika maendeleo na kwamba inafahamu
mchango wa Tanzania katika kuendeleza ushirikiano wa nchi za Afrika
Mashariki. Katibu Mkuu huyo pia aliongeza kuwa, Tanzania imemudu
kudumisha amani kwa kipindi kirefu huku ikipiga hatua za kimaendeleo na
kwamba watu wake wamebakia wamoja kwa miaka mingi licha ya kuwa na
tofauti za kitamaduni, kijiografia na kidini.
Kauli
hiyo ya Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Japan, imetolewa kufuatia
mkutano wake na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Mohammed Gharib Bilal ambaye yupo jijini Tokyo kwa ziara ya kikazi.
Katibu huyo alisema, “tunaifahamu Tanzania kama nchi muhimu inayodumisha
amani. Nchi yenu imeweza kudumisha Muungano kwa miaka 50, Japan
inawapongeza sana. Tunafahamu mnafanya kazi kubwa katika kuwaendeleza
wananchi wenu na sisi kama ndugu na rafiki zenu tuko tayari kabisa
kushirikiana nanyi.”
Katibu
Mkuu Suga alieleza pia kuwa, Tanzania ni nchi iliyo thabiti katika
ukanda wa Afrika Mashariki na inayo nguvu katika kuhakikisha ukanda huu
unaendeleza utengamano hali ambayo inachangia kuwepo maingiliano ya
wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki sambamba na kutanua fursa kwa
wawekezaji kutoka nje ya Afrika.
“Mko
thabiti katika mambo mengi na hasa kuweza kumudu kuwa na amani na
utulivu, mnategemewa sana na nchi za Afrika Mashariki na kwa hali hii
sisi tupo tayari kuendelea kutenga fedha katika bajeti yetu kwa ajili ya
kusaidia miradi mbalimbali ya Tanzania katika ushirikiano wa serikali
na sekta binafsi (PPP),” alisema.
Kwa
upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal alimueleza Katibu Mkuu
Suga kuwa, Tanzania inapokea kwa heshima kubwa mchango wa Japan kwa
kutambua hali yake ya utulivu na kwamba anatumia ziara yake Japan
kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania.
“Tuna
kazi kubwa mbele yetu katika kuwaendeleza Watanzania. Hatuwezi kufanya
kazi hiyo peke yetu, hivyo basi nitumie nafasi hii kukuomba Mheshimiwa
Katibu Mkuu kutusaidia kuhamasisha wawekezaji kutoka Japan ili waje
kushirikiana nasi katika kuiendeleza Tanzania. Urafiki kati yenu na sisi
ni wa siku nyingi na tungetegemea sasa tuubadili na utazame fursa za
kuchangiana kiuchumi na hasa katika kuwekeza kwa kubadilishana
teknolojia pamoja na mtaji,” Makamu wa Rais alisema.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais yuko nchini Japan kwa ziara ya kikazi na tayari
amefanikiw akukutana na wakuu wa makampuni mbalimbali makubwa duniani
yenye makao yake makuu nchini Japan na kisha kutumia nafasi hiyo
kuelezea fursa za uwekezaji nchini Tanzanja sambamba na kubainisha
umuhimu wa sekta binafsi kushiriki katika kusaidia maendeleo ya nchi
zinazoendelea zilizopo Afrika, Tanzania ikiwa ni kipaumbele.
No comments:
Post a Comment