Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika pamoja na
baadhi ya wananchi kuangalia athari iliyotokea na nyumba ya Bwana Salim
Ahmed Salim baada ya ukuta na dari yake kuanguka saa sita usiku juzi
mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Sehemu ya mbele ya Nyumba ya Bwana Salim Ahmed Salim iliyoporomoka Mtaa wa Vuga mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja.
Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana na athari hiyo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizungumza na Meneja wa Kampuni ya
Kimataifa ya uwekezaji vitega uchumi wa Kampuni ya Lucky Exports kutoka
Nchini India Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi
Seif akisalimiana na Menaja wa Kampuni ya Lucky Exports ya India
inayotaka kuwekeza katika sekta za Afya na Viwanda vidogo vidogo vya
mazao ya Baharini.
Balozi Seif akisalimiana na Mwakilishi wa Kampuni ya Lucky Exports Tawi la Tanzania Bwana Kim Mghaya. Kati kati yao ni Meneja wa Kampuni hiyo yenye makao makuu yake Nchini India Bwana Ravi Rai.
*********************************
Mamlaka
ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Jeshi la Polisi pamoja na
Mamlaka ya Usafiri zimekumbushwa kuendelea kuzuia uingiaji wa gari
kubwa zenye uzito wa zaidi ya Tani Mbili katika eneo la Mji Mkongwe ili
kunusuru majengo yaliyono ndani ya mamlaka hiyo.
Kumbusho
hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alipofanya ziara fupi kukagua athari ya nyumba iliyoporomoka
ukuta na Dari yake juzi usiku iliyopo Mkabala na Skuli ya Sekondari ya
Tumekuja Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi
Seif alisema ukaidi wa baadhi ya madereva wa gari kubwa kupitisha Gari
gari zao katika eneo hilo umesababisha uchafuzi wa mandhari na haiba ya
Mji mkongwe wa Zanzibar ambao hivi sasa uko katika urithi wa
Kimataifa.
“
Jeshi la Polisi wakati huu litahitajika kuwa na kazi ya ziada katika
kuhakikisha agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar
linatekelezwa ipasavyo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimpa pole Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana
Salim Ahmed Salim kwa hasara aliyoipata alimtaka kuwasiliana na
Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar katika juhudi
zaujenzi wa nyumba hiyo utakaozingatia mpango halisi wa uhifadhi wa
Mji huo.
Akitoa
ufafanuzi wa athari nyingi zilizojitokeza ndani ya nyumba za Mji
Mkongwe, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano na Utafiti cha Mamlaka ya
Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Bibi Madina Haji Khamis alisema
ujenzi usiozingatia utaalamu wa Mamlaka husika pamoja na upitishwaji wa
gari kubwa ndio sababu kubwa za msingi za athari hizo.
Bibi
Madina alifahamisha kwamba baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walikuwa
wakipandishia kuta wakati wa ujenzi au matengenezo zaidi ya uwezo wa
msingi wa nyumba hizo hali inayoleta athari ya mipasuko ya nyumba hizo
sambamba na mitetemeko ya gari kubwa zinazopitishwa pembezoni mwa nyumba
hizo.
Mapema
Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim Ahmed Salim alimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba dalili za kuanguka kwa
jengo hilo zilijionyesha mapema kutokana na kuvimba na baadaye kupasukwa
kwa eneo la mbele la ukuta wa nyumba hiyo.
Bwana
Salim alifahamisha kwamba kutokana na hali hiyo alilazimika kuuarifu
Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliolazimia
baadaye kwa kushirikiana na jeshi la Polisi kuchukuwa hatua za kuifunga
bara bara hiyo.
“
Nilijaribu kuufuata Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe
uniruhusu kuifanyia matengenezo makubwa nyumba yangu ili baadaye
niitumie kwa makazi na familia nyangu lakini bado sijapata jibu na huku
inaporomoka “. Alieleza Bwana Salim Ahmed Salim.
Nyumba
hiyo ya ghorofa moja mpaka inaporomoka ukuta na dari yake majira ya saa
sita juzi usiku lakini hamna watu waliokuwa wakiishi ndani yake.
Mamlaka
ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi nyengine
zimelazimika kuzuia Gari zote zinazotumia Bara bara hiyo kutoka Vuga
kuingia Shangani au kupitia Serena ili kujaribu kuepuka hatari katika
kipindi hichi cha Mvua za Masika.
Kwa
mujibu wa hali halisi ilivyo hivi sasa gari zote zinazokusudia kuingia
ndani ya eneo la Mamlaka ya Mji Mkongwe zinalazimika kutumia Bara bara
itokayo Malindi na zisizidi uzito wa zaidi ya Tani mbili.
Mamlaka
ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa imo ndani
ya Ramani ya Dunia ya urithi wa hifadhi ya Kimataifa chini ya usimamizi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni { UNESCO
}.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa
mazungumzo na ujumbe wa Kampuni ya uwekezaji vitega uchumi vya sekta za
Afya, Kilimo, Umeme, viwanda vidogo vya mazao ya Baharini ya Lucky
Exports kutoka Nchini India.
Kampuni
hiyo ambayo imefungua Matawi yake katika mataifa mbali mbali Barani
Afrika tayari imeshapata usajili wa kufungua Tawi lake Nchini Tanzania.
Katika
mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar Meneja wa Kampuni hiyo Bwana Ravi
Rai alisema Taasisi yake imelenga kutoa huduma za afya pamoja na
viwanda vidogo vidogo vya mazao ya Baharini.
Bwana
Ravi Rai alisema wakati Uongozi wa Taasisi yake ukisubiri kuanza na
hatimae kukamilisha taratibu zote za uwekezaji uwekaji wa miradi hiyo
umekusudia kusaidia kutoa ajira kubwa kwa wazalendo pamoja na kuongeza
mapato ya Taifa.
Alifahamisha
kwamba utafiti wa wataalamu wa Taasisi hiyo utafanywa ili kuangalia
miradi ambayo kampuni hiyo inaweza kuiwekeza hapa Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla.
“
Tunafarajika kuona kwamba miradi yoyote tutakayoamuwa kuitekeleza
kwenye uwekezaji wa mataifa mbali mbali duniani na hasa tukilenga zaidi
Bara la Afrika inafadhiliwa na Serikali ya India “. Alisema Meneja huyo
wa Lucky Exports.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema miradi iliyofikiriwa kuanzishwa na Uongozi wa Kampuni hiyo hapa
Zanzibar ya Sekta ya Afya na Viwanda Vidogo vidogo vya mazao ya
Baharini itasaidia kustawisha maisha naustawi wa Jamii Nchini.
Balozi
Seif aliuagiza Uongozi wa Kampuni hiyo ya Lucky Exports kutoka Nchini
India kurahisisha maombi yao ya uwekezaji ili taasisi zinazohusika na
uwekezaji ziweze kuyapitia na kutoa maamuzi yanayostahiki kwa wakati
muwafaka.
Kampuni
ya Uwekezaji ya Lucky Exports ya Nchini India ambayo tayari
imeshafungua matawi yake katika Mataifa ya Ethiopia, Guinea Bisau,
Malawi na Tanzania inajihusisha zaidi na uwekezaji wa miradi ya Afya,
Kilimo, Viwanda vya mazao ya Baharini, Umeme pamoja na huduma za Reli.
No comments:
Post a Comment