Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, December 17, 2014

Gwiji Shem Karenga afariki, kuzikwa leo Kisutu


Shem Ibrahim Karenga enzi za uhai wake.
MWANAMUZIKI mkongwe nchini aliyekuwa amejaliwa kipaji cha kuimba na kucharaza gitaa kiongozi la Solo, Shem Ibrahim Karenga amefariki dunia jana akiwa katika Hospitali ya Amana  jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa na anatarajiwa kuzikwa leo.
Marehemu Kalenga anayekumbukwa kupitia tungo zake mbalimbali zilizochangia kumpa umarufu, alizozifyatua akiwa na bendi mbalimbali kama vile ‘Tucheze Segere’, ‘Muna’, ‘Kila jambo’ na ‘Mbelaombe’, alifariki asubuhi ya jana wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
http://3.bp.blogspot.com/-JFXFWxOdnew/UOSAJukbR8I/AAAAAAAAAEM/Xh2poUooXFI/s1600/DSCN9027.JPG
Mzee Shem Karenga akiwa jukwaani enzi za uhai wake
Kwa mujibu wa Kiongozi wa bendi ya African Minofu, Joseph Matei, marehemu aliugua siku chache zilizopita kabla ya kukumbwa na mauti na kwamba anatarajiwa kuzikwa leo kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar. 
Gwiji hilo Shem Karenga alizaliwa mwaka 1950, Bangwe, Kigoma na kupata elimu ya msingi katika shule ya kimishionari ya Kihezya kuanzia mwaka 1957 hadi mwaka 1964.  
Mwaka 1964 alijiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz ambayo maskani yake yalikuwa mjini Kigoma. Mwaka 1972, aliitwa kwenye bendi ya Tabora Jazz kama mwanamuziki mwenye kipaji cha utunzi, mwimbaji na mpigaji wa gitaa la Solo. 
Mwaka 1983 alijiengua kutoka Tabora Jazz na kusimama kabisa kujihusisha na muziki, ambako kilichofuatia ilikuwa ni kifo cha bendi hiyo. 
http://3.bp.blogspot.com/-weZJKpIviOU/UOV5fzp6QxI/AAAAAAAAAcw/rMGIJd5BwoY/s1600/PICTURE+07.jpg
Shem Karenga akicharaza gitaa na kuimba kiasi cha kumkuna Mayaula Mayoni (kulia)
Mwaka 1990 aliondoka Tabora na kutua jijini Dar es Salaam. Mwaka 1990 alijiunga na MK Beats. 
Mwaka 1995, MK Beats ilisambaratika, ambako mwaka uliofuata, yaani 1996 alianzisha bendi ya Tabora Jazz Star kwa kushirikiana na Ibrahim Didi. Mpaka mauti yanamfika, Shem Karenga Mkurugenzi Msaidizi katika Bendi ya Tabora Jazz Star ambapo Mkurugenzi Mkuu ni Ibrahim Didi. Moja ya vibao vyake viliwahi kunyakuliwa na kurejewa na kundi la Sokousou Stars kuonyesha alivyokuwa mkali.
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia ya marehemu pamoja na wanamuziki na wadau wote wa fani ya muziki nchini kwa msiba huo.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU Mahali PEMA PEPONI.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...