Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, December 31, 2014

MAALIMU SEIF SHARIFF HAMADI AUNGURUMA UNGUJA


Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimpongeza Mhe. Mansour Yussuf Himid baada ya kuamua kujiunga na chama hicho na kumkabidhi rasmi kadi ya CUF katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini UngujaMKOA WA KUSINI UNGUJA.                              
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mansour Yussuf Himid, amejiunga rasmi na chama cha wananchi CUF.
Mhe. Mansour ambaye amewahi kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushika nyadhifa mbali mbali ikiwemo ya Waziri wa Kilimo, amechukua uamuzi huo leo kwenye mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Baada ya kukabidhiwa kadi ya CUF na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Mhe. Mansour amesema ameamua kujiunga na CUF baada ya kubaini na kuridhika kuwa chama hicho kimebeba matumaini mapya ya wazanzibari.
Mhe. Mansour ambaye tayari alishateuliwa na chama hicho kuwa mshauri wa mikakati wa Katibu Mkuu wa CUF, amechukua kadi hiyo akiwa miongoni mwa wanachama wapya 108 waliojiunga na CUF kwenye mkutano huo.
Mapema akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Mhe. Mansour kwa kuamua kujiunga na chama hicho hadharani, na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha kijasiri.
Akizungumzia mafanikio ya chama hicho, Maalim Seif amesema kimepata mafanikio makubwa katika mwaka unaomalizika wa 2014, na kutangaza maazimia mapya ya chama hicho kwa mwaka 2015.
Ametaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuendelea kukubalika kwa chama hicho katika pembe zote za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kuhusu maazimio ya Chama hicho kwa mwaka 2015, Maalim Seif amesema kimejipanga kuhakikisha kuwa kinashinda kwa asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu ujao na kuweza kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo amewataka wanachama wasibetweke kutokana na mafanikio yaliyopatikana, bali waongeze nguvu kuhakikisha kuwa malengo ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao yanafikiwa.
Ameongeza kuwa CUF pia kimejipanga kuimarisha uchumi na kujenga Zanzibar mpya itakayokuwa ya matumaini kwa Wazanzibari wote.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema katika uchaguzi mkuu ujao hatowazuia vijana kutetea haki yao iwapo watadhulumiwa.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 nilifanya kazi kubwa ya kuwazuia vijana wasifanye vurugu pale hoteli ya Bwawani. Mwanzo niliwatuma wasaidizi wangu waende kuwaondosha lakini hakuna aliyesikia hadi nilipokwenda mwenyewe, tena waliondoka kwa shingo upande kabisa. Kwa hivyo uchaguzi mkuu ujao sina namna yoyote ya kuwazuia vijana kutetea haki yao”, alifafanua Maalim Seif.
Kabla ya mkutano huo Maalim Seif alifanya ziara ya kukagua uhai wa chama hicho katika vijiji vya Michamvi, Bwejuu, Jambiani na Paje ambako aliweka mawe ya msingi kwenye matawi ya chama hicho, pamoja na kupandisha bendera kwenye barza ya DAY OUT ya Paje.
………………………………………………………………………………………

Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, baada ya  kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.

.   Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake , baada ya  kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.

.   Wanachama wa CUF wakionyesha kuunga mkono uamuzi wa Mansour Yussuf Himid kujiunga rasmi na chama hicho kwenye viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja. (Picha na Salmin Said, OMKR).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...