Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, December 27, 2014

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi asimamishwa kazi! Nani atakayefuata?!


http://2.bp.blogspot.com/-lNHMgYrosWI/Un0Grc2W8kI/AAAAAAAAAlA/Rpir-urB1J8/s1600/maswi-sept30-2013.jpg
Al;iyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
SAKATA la Akaunti ya Tegeta Escrow limeendelea kuzama na watu baada ya muda mfupi uliopita MICHARAZO kupata taarifa kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi  amesimamishwa kazi ili kupisha mamlaka kufanya uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili.
Kusimamishwa kwa Maswi kumekuja ikiwa ni simu moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jioni hii kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Tanzania inasema kuwa Katibu Mkuu Maswi amesimamishwa kazi.
Taarifa hiyo inasema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue amemsimamisha kazi kwa muda Ndugu Eliakim Maswi,  Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Uchunguzi huu ni moja ya hatua za utekelezaji wa maazimio nane yaliyotolewa na Bunge ambayo yalimtaka Rais Kikwete kuwawajibisha wahusika wote waliohusika na ubadhilifu wa pesa za Escrow.
Hii hapa taarifa kamili iliyotolewa na Kurugeni hiyo muda mfupi uliopita.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, amemsimamisha kazi kwa muda Ndugu Eliakim Maswi,  Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati na Madini, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Balozi Sefue amemsimamisha kazi Ndugu Maswi kuanzia leo, Jumanne, Desemba 23, 2014, kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema kuwa amechukua hatua hiyo “Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa)” ambapo “Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.”
Badala yake, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi C. Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, hadi uchunguzi dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi utakapokamilika.
Taarifa hiyo ya Balozi Sefue pia imekariri kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa jana, Jumatatu, Desemba 22, 2014 ambako Rais alisema:
“Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
Ndugu Maswi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Ndugu Frederick Werema pamoja na Mawaziri wawili walituhumiwa wakati wa Kikao cha Bunge kilichopita kuhusiana na Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati huo huo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa, Shirika la Umeme (TANESCO) waendelee na majadiliano na IPTL kuhusu uwezekano wa kushusha tozo la uwekezaji (capacity charge) zaidi ya punguzo la awali lililopatikana kupitia Kituo cha Kimataifa cha Kusuluhisha Migogoro ya Kimataifa (ICSID).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
23 Desemba, 2014

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...