Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, December 22, 2014

SERIKALI YAZINDUA RASMI USAMBAZAJI TAKWIMU ZA PATO LA TAIFA, PATO LA MWANACHI LAONGEZEKA


 Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya Salum (katikati) akizindua rasmi   Takwimu za Pato la Taifa zilizorekebishwa kwa mwaka wa kizio wa 2007 jana jijini Dar es salaam. 
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa(Kushoto) akitoa ufafanuzi wa kazi ya kurekebisha takwimu za Pato la Taifa iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliyotumia tafiti za taifa zilizofanyika kwa kipindi cha mwaka 2001 hadi 2007.Kulia ni Waziri wa Fedha Mh. Saada Salum Mkuya.
Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya Salum (kulia) akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servicius Likwelile chapisho la lenye Takwimu za Pato la Taifa zilizorekebishwa kwa mwaka wa kizio wa 2007 wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa takwimu hizo leo jijini Dar es salaam.
::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.Dar es salaam
Serikali imesema kuwa Pato la Taifa kwa mwaka 2007 limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 26.8  ikilinganishwa na trilioni 20.9 za mwaka 2001, ambapo wastani wa pato la mwananchi mmoja mmoja limeongezeka kutoka shilingi milioni1,186,200/= mwaka 2001 hadi shilingi milioni 1, 561,050/= mwaka 2013.  
 Akizindua usambazaji wa takwimu hizo leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya Salum ameeleza kuwa matokeo hayo  ni sawa na ongezeko la ukubwa wa Pato la Taifa kwa asilimia 27.8.  
Amesema ongezeko hilo ni matokeo ya juhudi za Serikali kuweka mazingira mazuri na kutengeneza  fursa za kuwawezesha wananchi kufanya kazi za kujiajiri na hatimaye kupata kipato halali kwa kazi wanazofanya. 
Mh. Mkuya amesema kuwa kukua kwa uchumi wa Tanzania kumechangiwa na kujumuishwa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo Sayansi na Teknolojia ambako kumetoa fursa kwa wananchi kujiongezea kipato hususan matumizi ya simu za kiganjani ambazo zimerahisisha mawasiliano na utafutaji wa masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi.
Amezitaja shughuli nyingine kuwa ni ukamilishaji wa miamala mbalimbali ya kibenki na mikopo ambazo zimekuzwa  na sekta ya mawasiliano , kuongeza ajira  na kupunguza muda wa kusubiri huduma za malipo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, amefafanua kuwa kuongezeka kwa thamani ya Pato la Taifa kunaiongezea Serikali uwezo kimapato kupitia kodi na kuiwezesha kugharamia ujenzi wa miundombinu na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, utafiti wa mapato na matumizi ya Kaya Binafsi ya mwaka 2012 unaonyesha asilimia 60 ya kaya zote nchini zinapata maji safi na salama hasa hususan maeneo ya mijini,zaidi ya asilimia 20 ya kaya zote nchini zinatumia nishati umeme haya ni mafanikio makubwa ya matokeo ya ukuaji wa uchumi nchini” Amesisitiza Mh. Mkuya. 
Akizungumzia mchango wa Sekta Binafsi katika kukua kwa pato la taifa nchini amesema kuwa ajira zipatazo laki nne kati ya laki sita  katika sekta iliyo rasmi zimepatikana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza wakati wa  uzinduzi huo amesema  kuwa kazi ya kurekebisha takwimu za Pato la Taifa imetumia Tafiti za Taifa zilizofanyika kwa kipindi cha mwaka 2001 hadi 2007.
Amezitaja tafiti hizo kuwa ni pamoja na utafiti wa mapato na matumizi ya Kaya wa mwaka 2007, Sensa ya Kilimo iliyofanyika mwaka 2008 na Takwimu nyingine za utawala kutoka katika Wizara na Idara za Serikali.
Aidha, amefafanua kuwa ukokotoaji wa takwimu hizo umefuata mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kutayarisha takwimu za Pato la Taifa wa mwaka 1993 na 2008 kwa lengo la kuhakikisha kuwa takwimu hizo zinalinganishwa na takwimu nyingine duniani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...