Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, July 8, 2012

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KWA MBUNGE WA BUMBULI JANUARY MAKAMBA



Napenda kuwatangazia wana-Bumbuli kwamba ile ahadi niliyotoa wakati wa kampeni – ahadi ya kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli – imetimia.  Shirika limepata usajili, limefungua ofisi, lina watumishi wa mwanzo na tayari ipo miradi minne ambayo utekelezaji wake utaanza mara moja. Tutazindua Shirika hili tarehe 4 Agosti 2012, katika mkutano wangu na wana-Bumbuli waishio Dar es Salaam na mikoa ya jirani, na baadaye katika mikutano na wananchi jimboni Bumbuli.
Chimbuko
Nilipoamua kugombea Ubunge wa Bumbuli mwaka 2010, niliamua kwamba katika utumishi wangu kama Mbunge nitashirikiana na Wana-Bumbuli pamoja na marafiki na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii Bumbuli. Jimbo letu ni kati ya majimbo yaliyo nyuma kimaendeleo kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhitaji jitihada za ziada – zaidi ya zile za Serikali. Katika kufikia lengo hilo, niliahidi kuanzisha Shirika litakaloratibu shughuli za maendeleo katika Jimbo.
Nilifikia uamuzi wa kuanzisha Shirika nikitambua kwa dhati uwepo wa  jitihada nzuri za serikali katika kuboresha maisha ya watu wa Bumbuli nikitegemea pia serikali kuendeleza jitihada zaidi. Hata hivyo natambua kwamba kazi ya maendeleo si kazi ya serikali pekee, inahitaji ushiriki wa kila mmoja na hasa sekta binafsi ili kuisadia juhudi za serikali kufikia malengo ya maendeleo. Nilitaka kuchambua uwezo wa watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali katika kupanua wigo wa ajira na shughuli za kipato kwa watu wa Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii.
Mpango wa Mageuzi Bumbuli
Mpango huu ulitokana na mawazo niliyokuwa nayo nilipoamua kugombea ubunge juu ya haja kuunganisha jitihada za wenyeji wa Bumbuli, wafanyabiashara na taasisi za hapa nchini, na wawekezaji kutoka nje katika kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Niliamini jitihada za sekta binafsi  zikioana na mipango ya maendeleo ya serikali kutachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa wana-Bumbuli na hivyo kupanua wigo wa ajira na shughuli za kibiashara za uzalishaji mali katika Jimbo.
Malengo ya mpango wa kuikwamua Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii ni kama ifuatavyo:
    1. Kuongeza pato la wakulima wa Bumbuli kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha mbinu za kilimo, mbinu za kuhifadhi mazao, na hatua mahsusi za kuongeza thamani ya mazao hayo (value-addition).
    1. Kuwavutia wawekezaji kujenga taasisi au shule itakayokuwa na wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa Bumbuli, hivyo kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
    1. Kuleta huduma za kifedha kwa kuanzisha taasisi ya fedha Bumbuli ambayo hatimaye itakuwa benki ya wananchi wa Bumbuli ambayo itatoa mikopo kwa masharti nafuu.
    1. Kuchukua hatua mahsusi za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani maisha na maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Bumbuli yanategemea sana mazingira na mandhari ya milima ya Usambara.
    1. Kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli litakalokuwa na jukumu la kubuni, kuratibu na kusimamia uendeshaji wa shughuli zilizoainishwa hapo juu. Shirika hili ndilo litakalokuwa kiini cha mtandao wa kijamii wa uchumi kwa Bumbuli.
Malengo haya yamekusudiwa kuwanufaisha wananchi kwa kuanzisha mtandao wa kimataifa wa kibiashara ambapo wadau mbalimbali watashiriki; na hatamu za uchumi zikishikiliwa na watu wa Bumbuli wenyewe.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...