Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, July 27, 2013

TANZANIA YATOLEWA MICHUANO YA CHAN


Tanzania (Taifa Stars) imeshindwa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kwa mara ya pili mfululizo baada ya leo (Julai 27 mwaka huu) kufungwa mabao 3-1 na Uganda Cranes, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1.
Stars ambayo ilicheza fainali za kwanza zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009 ilimaliza kipindi cha kwanza katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Kampala ikiwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji ndiyo walioanza kufunga bao dakika ya saba katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar. Frank Kalanda alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa ndani ya eneo la hatari la Tanzania.
Bao hilo halikuonekana kuichangaza Taifa Stars, kwani ilitulia na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 18 mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana na pasi nzuri ya Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.
Dakika ya 32 nusura Taifa Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Mrisho Ngasa ambao tayari ulikuwa umempira kipa HAmza Muwonge uligonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Uganda Cranes.
Mabao mengine ya Uganda Cranes yalifungwa dakika ya 48 kupitia kwa Brian Majwega na lingine dakika ya 63 mfungaji akiwa tenda Kalanda kutokana na makosa ya Salum Abubakar kupokonywa mpira wakati akiwa katika nafasi nzuri ya kutoa pasi kwa mwenzake.
Kocha Kim Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43 kwa kumuingiza Simon Msuva badala ya Frank Domayo aliyeumia, na dakika ya 78 akawaingiza kwa mpigo Haruni Chanongo na Vincent Barnabas badala ya David Luhende na John Bocco. Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani kesho (Julai 28 mwaka huu) saa 4 usiku kwa ndege ya PrecisionAir.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Kampala

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...