Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, July 14, 2013

MECHI YA TAIFA STARS, UGANDA YAINGIZA MIL 113/-


Kikosi cha Stars

Mechi ya kwanza mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) iliyochezwa jana (Julai 13 mwaka huu) imeingiza sh. 113,268,000 kutokana na watazamaji 17,121.
Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 17,278,169.49 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 7,809,104.
Asilimia 15 ya uwanja sh. 13,227,108.98, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 17,636,145.30 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 4,409,036.33.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 52,908,435.91 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,645,421.80 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
TAIFA STARS KAMBINI TENA JULAI 4
Timu ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka leo asubuhi (Julai 14 mwaka huu) kwenda Mwanza ambapo itapiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Uganda (The Cranes) kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeondoka kwa ndege ya PrecisionAir na itafikia hoteli ya La Kairo wakati mazoezi yatafanyika Uwanja wa CCM Kirumba kulingana na programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen.
Wachezaji walioko katika kikosi hicho ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Tarehe rasmi itapangwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Uganda (FUFA) siku kumi kabla ya mechi.
TENGA AWASHUKURU WAJUMBE WA MKUTANO MKUU TFF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa michango yao, na utulivu waliouonesha katika kupitisha marekebisho ya Katiba ya TFF ya 2013.
Amesema marekebisho hayo yatawasilishwa kesho (Julai 15 mwaka huu) kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kupitishwa ili mchakato wa uchaguzi uweze kuanza mara moja.
“Tutamuomba Msajili atusaidie kusajili haraka Katiba yetu ya 2013 ili tuingie katika mchakato wa uchaguzi. Kama tulivyotangaza awali tumepanga kufanya uchaguzi Septemba 29 mwaka huu, na tusingependa tarehe hiyo ipite,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji.
Katika kikao chake, Kamati ya Utendaji  imepitisha Kanuni za Maadili, Kanuni za Nidhamu, na marekebisho kwenye Kanuni za Uchaguzi yanayotokana na kuundwa kwa Kamati ya Maadili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...