Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, July 17, 2013

TANESCO YASAINI MKATABA WA NISHATI YA UMEME NA KAMPUNI YA CPI


 Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba akisaini hati na Mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji ya CPI, Lu Quizhou baada ya kuingia mkataba wa uwekezaji wa nishati ya Umeme jijini Dar es Salaam leo. 
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba akibadilishana hati na Mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji ya CPI, Lu Quizhou baada ya kuingia mkataba wa uwekezaji wa nishati ya Umeme kutoka China. 

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameendelea kusisitiza na kuwataka wakazi wa mkoa wa Mtwara kuelewa kuwa Gesi iliyopatikana katika mkoa huo ni kwa ajili ya Watanzania wote.

Akizungumza wakati akiwekeana makubaliano na kampuni ya uwekezaji wa nishati ya umeme kutoka China (CPI), Profesa Muhongo alisema kuwa hata kama wakazi wa mkoa huo watashindwa kuridhia uwekezaji wa nishati hiyo lakini gesi hiyo ni kwa maendeleo ya Watanzania wote.

Profesa Muhongo alisema kuwa makundi yanayopinga matumizi ya gesi hiyo yanapaswa kuweka hadharani mikakati yao kuliko wanavyofanya sasa kwa kupinga pasipo kutoa mipango yao.

Alisema inapaswa kufika mahali Watanzania wakagawanywa katika makundi mawili ikiwemo lile linalotaka maendeleo na linalopinga ili waweze kutengewa maeneo.

“Hatuwezi kuondoa umaskini kama tusipotumia gesi na raslimali tulizo nazo na hata hili tatizo linalolalamikiwa sasa la vijana kukosa ajira litapata ufumbuzi kama tutaweza kupanua uchumi wetu,” alisema.

Alisema kuwa Watanzania wanapaswa waache kulazimisha kufuata mawazo ya kupotosha.

“Tunataka uchumi ukue, tuwe na umeme wa uhakika na hata bajeti yetu kuondoka katika kuongeza bei katika bidhaa ndogo ndogo ili linaweza kufanikiwa kama tukiwa na umeme wa uhakika na kutumia gesi yetu,” alisema.

Aidha katika makubaliano hayo, Serikali imeingia makubaliano na kampuni hiyo kwa kuzalisha umeme wa megawati 600 katika eneo la Kinyerezi namba 3 lililopo jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa umeme huo utatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ifikapo mwaka 2014 mwishoni wataweza kuuza megawati 500 kwa nchi za nje zenye uhitaji wa nishati hiyo.

“Kupitia uzalishaji huo tunategemea mwaka 2016 tutaweza kuzalisha megawati 1500 za nyongeza  hatua hiyo itaweza kubadilisha uchumi wetu na kuwa na bajeti yenye uhakika zaidi,” alisema.


Profesa Muhongo alisema kuwa makubaliano hayo ambayo yanafanyika na Shirika la Umeme Nchi (Tanesco) na kampuni hiyo ya CPI utaweza kugharimu kiasi cha Dola milioni 300 hadi kukamilika.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...