Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, July 28, 2013

Kikwete; Umepokea Malalamiko ya Chadema!


Na Bryceson Mathias
HIVI karibuni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilidai kamwe hakitakabidhi ushahidi kwa Jeshi la Polisi nchini kuhusu Askari aliyehusika na Bomu la Arusha hadi Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume ya kijaji.
Watanzania nikiwepo mimi wamekuwa na uchu wakisubiri kutaka kujua kauli ya Rais Kikwete iwapo ni kweli amepokea Malalamiko ya Chadema! Na je, kukaa kimya ameyakubali au laa?.
Hamu na Uchu wa watanzania kutaka kujua mustakabali wa jambo hilo, ni kutokana na kwamba, tukio hilo liliua watu watu wane na wengine zaidi ya sitini kujeruhiwa, lakini pili ni kutokana na msimamo wa Chadema kutotaka kutoa ushahidi polisi hadi Kikwete aunde tue ya Kijaji.
Takribani mara mbili sasa, Mwenyekiti wa chadema, Freeman Mbowe, baada ya kuhojiwa makao makuu ya polisi, akizungumza na wandishi wa habari Dar es salaam, amerudia kauli yake akisema,

 “Msimamo wa chama chetu, ni kwamba hatutatoa ushahidi polisi hadi Rais Kikwete atakapounda tume ya kijaji, na hii ndo kauli kubwa niliyowaambia polisi nilipohojiwa.


“Nimewaaleza tukiwa kama chama tulishamwandikia barua Rais Kikwete ya kuunda tume ya kijaji ya kimahakama na yeye bado hajajibu kama amekubali au laa.
“Sisi tutaendelea kusubiri kauli ya Rais Kikwete kama ataunda tume leo hata kesho, tupo tayari kupeleka ushahidi tulionao,”alisisiza Mbowe.
Alisema baada ya kauli hiyo, maofisa wa polisi wakita CHADEMA kupeleka ushahidi wao kwa maandishi.
“Polisi wametuomba, tuweke uamuzi wetu kwenye maandishi na tuyawasilishe siku ya Ijumaa, wakili wangu Peter Kibatala ameahidi kufanya hivyo,”alisema Mbowe.
Alisema mambo mengi aliyojadiliana na polisi, ni ya kisheria zaidi, hiyo wakili Kibatala atayaweka kwenye mtiririko na kuyawasilisha.
Julai 15, mwaka huu Mbowe alijisalimisha polisi saa 8.00 mchana na kuhojiwa na kikosi maalumu cha makachero wa jeshi hilo.

Hatua ya Mbowe kujisalimisha, ilitokana na taarifa kuwa polisi ilivamia nyumbani kwake saa 6.00 usiku Julai 14, mwaka huu kwa lengo la kumkamata.
Vyanzo vya kuaminika kutoka makao makuu ya polisi, vilivyotaka visitajwe vilisema Mbowe alihojiwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za uchochezi aliodaiwa kufanya kwa kuwa katika hotuba zake anajenga chuki kati ya wananchi na polisi.
Tuhuma nyingine, ni kauli aliyowahi kuitoa kuwa polisi inahusika katika tukio la mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15, mwaka huu CHADEMA walipohitimisha mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo viwanja vya Soweto Arusha.
Katika tukio hilo, Mbowe alidai Chadema kina ushahidi wa kutosha kuwa polisi wanahusika na tukio hilo kutokana na kuwa na mkanda wa video unaoonyesha tukio zima.
Tuhuma nyingine, ni ile ya kwamba kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutohudhuria mazishi ya watu waliofariki dunia katika mlipuko huo, kilihusishwa moja kwa moja kuwa ni ishara ya jeshi hilo kuhusika katika mauaji hayo.
Mbali na Kauli ya Mbowe kuwa na Ushahidi wa tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwiguliu Mchemba na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walidai wana ushahidi Chadema walijilipua.   
Ni rai yetu ili kuwafuta machozi watanzania, Rais aunde tume hiyo tumjue ni nani Mbaya wa vifo vya ndugu, Jamaa na Nguvu kazi ya Taifa letu.
nyeregete@yahoo.co.uk  0715933308

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...