Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa mkoa wa Lindi
kuhakikisha kuwa vijana wao wanaishi maisha ya uadilifu,
wanamcha Mwenyezi Mungu na kusoma elimu ya Dunia ili wasipotee katika
Ulimwengu wa utandawazi.
Mama
Kikwete ametoa wito huo jana wakati wa futari
iliyowajumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa
mkoani Lindi.
Alisema
kuwa ni jambo jema kwa binadamu kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi
Mungu kwani hatuna mtu anayejua siku yake ya kufa hivo basi ni muhimu
kujiandaa mapema kwa kutenda matendo mema ili ukifika huko uwe na
mazingira mazuri ya baadaye na hakuna cha kusema kuwa mimi ni mdogo
bado kwani kwa Mungu hakuna cha mdogo wala mkubwa.
“Kufunga
kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ni lazima kwani ni moja ya ibada
katika kutengeneza afya ya mwili wako na kuwa karibu na Mwenyezi Mungu
na ndiyo maana hata watoto wadogo wanatakiwa kujifunza kufunga.
Lakini
siku hizi kufunga imekuwa ni mtihani kwa baadhi ya watu kuna wengine
wanasingizia ugonjwa ili wasifunge jambo ambalo si sawa kwani kuna
baadhi ya watu wanaugua ugonjwa wa kisukari na wanafunga lakini hawapati
matatizo kwakuwa ukidhamiria utafunga tu bila tatizo hata kama
ni mgonjwa na Mwenyezi Mungu atakupa uzima”, alisema Mama Kikwete.
Aidha
Mama Kikwete pia aliwataka viongozi hao wa Serikali na vyama vya Siasa
kutunza amani iliyopo kwakuwa amani ni tuzo ya taifa na nchi bila ya
kuwa na amani haikali na hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika
kwani hata wanyama watapata tabu na kukosa mahali pa kuishi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila alimshukuru Mama
Kikwete kwa futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa dini zote
zinahimiza umuhimu wa kusali na kutubu hivyo basi ni jukumu la kila mtu
kufanya hivyo.
Mkuu
wa mkoa huyo alisema kuwa kila mtu anatakiwa kumcha Mungu na kumtukuza
bila kusahau kuwasaidia watu waliopo katika dhiki ambao wanatakiwa
kusaidiwa kwa kufanya hivyo watapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Naye
Shekhe na Kadhi mkuu wa mkoa wa Lindi Mohamed Mushangani alisema kuwa
utaratibu wa watu wa aina mbalimbali kukutana na kufanya jambo kwa
pamoja kunawafanya wapendane zaidi kwani mtu akikupenda nawe utampenda,
hivyo basi wawe na mapenzi na kupendana ili wapate raha katika maisha.
Alisema
kuwa katika kumi la pili la kufunga ni la msamaha kama alivyosema Mtume
Swalallahu Alayhi Wassalam (S.A.W) hivyo basi kwa wale wanaofunga
wanatakiwa kujikita zaidi katika kufanya mambo mazuri kwa watu ikiwa ni
pamoja na kulisha wengine kwani ukimpa kula na kunywa mwenzako Mwenyezi
Mungu anakulipa zaidi.
No comments:
Post a Comment