Bondia
wa kimataifa wa Namibia Gottlieb Ndokosho (kushoto) akiwa katika moja
ya mapambano yake. Ndokosho anatarajia kupanda ulingoni jijini Windhoek,
kupambana na Mtanzania Rajabu Maoja kuwania ubingwa wa IBF
Na Elizabeth John
BONDIA
Rajabu Maoja amejinadi kuhakikisha anarudi na ushindi katika pambano
lake na ubingwa wa IBF dhidi ya Mnamibia, Gottlieb Ndokosho katika
pambano linalotarajiwa kufanyika Septemba 29, mwaka huu katika jiji la
Windhoek, Namibia.
Akizungumza
kwa njia ya simu akiwa mkoani Tanga, alikoweka kambi, Maoja alisema,
katika pambano hilo lililopewa jina la ‘Vita ya jangwa la Kalahari’
amejipanga kuhakikisha anawapa raha Watanzania kwa kurudi na ubingwa
kwani ana imani atarudi nao.
“Nipo
huku Tanga ambapo ndiyo nyumbani lakini pia ndipo nilipoweka kambi
yangu hadi siku nitakayokwenda katika shindano, nimejipanga kuhakikisha
nanyakua ubingwa ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi kwani rekodi yangu
ni nzuri tofauti nay a mpinzani wangu na nimejiandaa vizuri kipindi
chote tangu nipate taarifa ya pambano hili,” alisema.
Pambano
hilo litasimamiwa na rais wa IBF katika Bara la Afrika, Mashariki ya
Kati, Ghuba ya Uarabuni na Ghuba ya Uajemi, Onesmo Ngowi huku
akishirikiana na Bodi ya Ngumi na Mieleka ya Namibia.
Kwa
upande wake Ngowi alisema, mapambano hayo yanatambuliwa na IBF yapo
katika mpango wa programu ya ‘Utalii wa michezo’ ambao IBF na USBA
umeufadhili na kuuendesha katika bara la Afrika huku Tanzania na Ghana
zikiwa ni nchi za majaribio katika mpango huo.
Aliongeza
kuwa programu hiyo, itawapa mabondia wengi wa Kitanzania nafasi
nyingine ya kugombea mkanda wa IBF sehemu mbalimbali duniani na
kuitangaza Tanzania.
No comments:
Post a Comment